December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NHIF yafunguka mafanikio ya Rais Samia kwa miaka mitatu

Na Jackline Martin,Timesmajiraonline,Dar

UONGOZI wa Rais Samia Suluhu Hassan, umewezesha sekta ya afya kupata mafanikio makubwa kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), ambapo umeendelea kuboresha kitita chake na kutoa kitita cha mafao chenye wigo mpana ikilinganishwa na skimu zingine za Bima ya Afya.

Maboresho hayo yametokana na uwekezaji mkubwa uliofanyika katika miundombinu na wataalamu katika sekta hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia.

Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi Mkuu NHIF, Bernard Konga, wakati akizungumza na wahariri na wa vyombo vya habari kuhusiana na mafanikio ya mfuko huo katika kipindi cha miaka miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia.

Akifafanua zaidi kuhusu ugharamiaji wa huduma za ubingwa bobezi, Konga alisema gharama za saratani kwa mwaka 2022/23 zilikuwa sh. Bilioni 32.46 ukilinganisha na sh. Bilioni 12.25 kwa mwaka 2021/22, pia gharama za matibabu ya figo zilikuwa sh.Bilioni 35.40 na sh. Bilioni 11.45.

“Lengo la kuboresha kitita ni kuimarisha upatikanaji wa huduma kwa kuzingatia mahitaji halisi ya tiba kwa sasa, kuwianisha miongozo ya Tiba nchini na kitita cha mafao kutekeleza mapendekezo ya taarifa ya thamani ya uhai wa mfuko ya mwaka 2021, ambapo mambo ya msingi yaliyozingatiwa.

Alisema mambo hayo ni pamoja na kufanya tafiti na uchambuzi wa gharama halisi katika soko la huduma za afya nchini, lakini pia kuwezesha huduma za kibingwa na ubingwa bobezi kufanyika katika hospitali ngazi ya Kanda .

Aidha, Konga alisema wamefanikiwa kuboresha huduma kupitia mikopo kwa watoa huduma, ambapo lengo ni kuendelea kutoa huduma bora kwa wanachama na wananchi kwa ujumla.

“Aina ya mikopo itolewayo ni pamoja na ujenzi na ukarabati wa majengo, vifaa tiba, dawa na vifaa vya TEHAMA,” alisema

Konga alisema katika kipindi cha mwaka 2021/22 hadi 2023/24 mfuko umetoa zaidi sh. Bilioni 24.4 kwa jumla ya vituo 29, lakini pia tangu kuanzishwa kwa utaratibu huo, mwaka 2007 jumla ya vituo 408 vimepokea mikopo yenye thamani ya sh. Bilioni 222.48.

Kuhusu utoaji elimu kwa umma, Konga alisema wamefanikiwa kutekeleza mpango wa uhamasishaji wa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kupima afya ili kujiepusha na magonjwa yasiyo ya kuambukiza, kutoa elimu kupitia mitandao ya kijamii.

Mbali na hayo Konga alizitaja changamoto ambazo wanakumbana nazo ikiwemo wananchi kutokuwa na utamaduni wa kuwa na Bima ya Afya, kuongezeka kwa magonjwa sugu yasiyo ya kuambukizwa na gharama zake, kuongezeka kwa gharama za matibabu nchini, lakini pia uhiari wa kujiunga kwa baadhi ya makundi ya wananchi