November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Dodoma yaanza kutumia kitita kipya cha NHIF

Zena Mohamed,TimesmajiraOline,Dodoma

HOSPITALI ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma imesema tayari imeshahamia kwenye kitita kipya cha mafao cha mwaka 2023 kilichopendekezwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa wote(NHIF)na huduma zinaendelea kutolewa kama kawaida.

Hayo yamesemwa jijini hapa leo,Machi 1 2024 na Mganga mfawidhi Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma na Mwenyekiti wa waganga wafawidhi Hospitali za Rufaa zote 28 za mikoa Tanzania bara Dkt.Ibenzi Ernest.

Dkt Ibenzi ameeleza kuwa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma kama mmoja wa watoa huduma hapa nchini wamejipanga vyema kutoa huduma bora kwa wananchi na itaendelea kufuatia utendaji wa kitita hicho ili kubaini changamoto zitakazojitokeza na kuziwasilisha katika Mamlaka husika ili kuendelea kutoa huduma zilizobora kwa wananchi.

Aidha amesema kuwa Hospitali hiyo imeboresha huduma mbalimbali ikiwemo madaktari bingwa kufanya kazi saa 24 pamoja na kuongeza muda wa wagonjwa wanaokwenda kwajili ya kliniki ya magonjwa mbalimbali kutoka muda wa awali ambao ulikuwa mwisho saa tisa alasiri.

“Awali wagonjwa wanaokuja kwajili ya kuwaona madaktari kwa kliniki mbalimbali walikuwa wanawaona mwisho saa tisa alasiri lakini sasa hivi daktari anawaona wagonjwa hadi watakapoisha,”amesema Dkt.Ibenzi.

Hata hivyo alizingumzia mpango wa Hospitali hiyo kuhusu wanachama wanaotumia bima za NHIF,kutokana na baadhi ya Hospitali za binafsi nchini kusitisha huduma kwa wanachama hao kuanzia leo Machi 1,2024,ameeleza kuwa
kuwa katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma kutakuwa na Mpango wa dharura wa utoaji huduma .

“Uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma umekuja na Mpango wa dharura wa kutoa huduma kwa wanachama hao ili waweze kuwa na mwendelezo wa huduma hizo kwani sisi kila siku tumejiandaa vizuri kutoa huduma kwa ubora,”ameeleza

Amesema kuwa hospitali hiyo inawagonjwa wengi ikiwemo waliopangwa kufanyiwa upasuaji na wao kama hospitali wanavyumba vya kutosha vya upasuaji,wanazo mashine za Kutosha na wameongeza zamu za kutoa huduma kwa wateja.