Mwandishi wetu, TimesMajira Online
KAMATI ya Kupitia Kitita cha Mafao cha NHIF cha mwaka 2023 imewatoa hofu watanzania kuwa hakuna atakayekosa matibabu kwa kuwa mkataba baina ya mfuko na watoa huduma za afya wa sekta binafsi (APHTA) haujavunjwa.
Hayo yamebainishwa Jijini Dar es salaam leo Februari 29 na Mwenyekiti wa kamati hiyo Dkt Baghayo Saqware wakati akizungumza na waandishi habari ambapo amesema kamati ilikuwa huru kumsikiliza kila mtu na walikubaliana kwa pamoja na kuamua kitita kianze kutumika kwa faida ya pande zote.
“Nawahakikishieni hakuna mtoa huduma atavunja mkataba na NHIF, tunahitaji mfuko uwe endelevu na wenzetu waliowekeza wawe endelevu, sisi tuko tayari kusikiliza kwa hoja kwanini wanasema wanapata hasara…wasitie watu hofu kama mtu anahisi hiki kitita hakitaki asilete taharuki haya ni mambo ya mkataba,” amesema Dk. Saqware.
Dkt Saqware amesema ujio wa Kitita hicho ni matokeo ya makubaliano ya pande zote ambazo ni watoa huduma binafsi za Afya na BAKWATA kwa maslahi ya serikali na sekta binafsi.
Aliongeza kuwa kamati hiyo ilitumia vigezo vyote kushughulikia malalamiko ya watoa huduma hao na hawajamwonea mtu yeyote, .
“Bei zetu sasa zina vigezo ambavyo vilikubaliwa kwa pamoja tuliwashirikisha. Huduma zitaendelea kutolewa kwa sababu mkataba na APHTA haujavunjwa”amesema Dkt Saqware
Vilevile Dkt Saqware amesema maboresho ya kitita cha mafao cha mwaka 2023 yalianza tangu mwaka 2018 kufuatia maelekezo yaliyotolewa na Wizara ya Afya iliyoelekeza mfuko kufanya mapitio ya kitita na bei zake kwa kuzingatia mwongozo wa matibabu nchini toleo la mwaka 2017.
Aidha kamati hiyo imeitaka Wizara kupitia NHIF iendelee na utekelezaji wa kitita cha mafao kilichoboreshwa cha NHIF cha mwaka 2023 kama walivyoshauri na kusisitiza kama itatokea mwanachama akakosa huduma atoe taarifa katika mamlaka husika.
Awali kitita hicho kimepangwa kuanza kutumika Machi Mosi,2024 lakini APHTA walikaririwa na vyombo vya habari wakisema watashindwa kutoa huduma kwa kuwa mazungumzo yao na kamati hayakufikia muafaka.
More Stories
Mchengerwa:Rufaa 5,589 za wagombea zimekubaliwa
Muhimbili yatoa orodha ya Majeruhi ajali ya kuporomoka kwa jengo kariakoo
RC Mtambi awataka Maofisa kilimo kutoa elimu ya kilimo mseto