Na Penina Malundo, timesmajira
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA)wamekutana kwa ajili ya kujadiliana kuhusu mashirikiano baina ya Taasisi hizo mbili ili kurahisisha zaidi utoaji wa huduma kwa wadau.
Akizungumza wakati wa kutambulisha ujumbe wa BRELA, kwa Mkurugenzi wa Dawa za Binadamu na Mifugo wa TMDA, Yona Mwalwisi, Msajili MsaidiI Mkuu wa BRELA Seka Kasera amesema kuwa mazungumzo hayo yataleta tija na ufanisi baina ya Taasisi hizo mbili ikiwa ni pamoja na kuondoa migogoro ya Wamiliki wa Alama za Biashara na Wamiliki wa Majina ya Dawa.
Ameendelea kusema kuwa BRELA na TMDA watakuwa na majadiliano ya pamoja ambayo yatawakutanisha wataalamu kutoka Taaisi hizo kwa ajili ya kuangalia na kubaini kwa pamoja maeneo ya kisheria na ya kiutendaji yenye kuonekana kuwepo kwa muingiliano wa majukumu ili kuweka mikakati ya pamoja ya kuondokana na mkanganyiko na muingiliano huo ili kurahisisha utoaji wa huduma hasa katika sajili za Alama za Biashara na Huduma na utekelezaji wa usajili na usimamamizi wa vifaa tiba na dawa mbalimbali.
Kasera amepambanua kuwa kikao kazi hicho baina ya BRELA na TMDA ni muendelezo wa utekelezaji wa mpango kazi wa Wakala wa kuimarisha mashirikiano na Taasisi za udhibiti nchini ili kuondoa changamoto hususan za kisheria ambazo zimekuwa zikijitokeza wakati na baada ya utoaji wa huduma.
“Katika kutelekeza majukumu yetu tunapaswa kushirikiana ili kutoa huduma za haraka na rafiki ukizingatia umuhimu wa taasisi hizi, TMDA mkisimamia dawa na vifaa tiba na BRELA tukiwa upande wa urasimishaji wa biashara, ambapo eneo la kufanikisha zaidi ni Alama za Biashara na Huduma sambamba na vumbuzi mbalimbali zinazohusiana na dawa na vifaa tiba ziweze kulindwa kisheria ili tunufaike kwa pamoja kama nchi” amesisitiza Bw. Kasera.
Aidha, ameongeza kuwa BRELA na TMDA katika kikao hicho watapitia maeneo yote yenye mwingiliano wa kimajukumu na kuyaweka sawa ili kumuondolea usumbufu mteja pale anapotaka huduma na hii itachochea uwekazaji zaidi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Dawa za Binadamu na Mifugo Mwalwisi, amemshukuru Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA kwa kuibua wazo hili ambalo litachangia katika kujenga mazingira rafiki kwa wafanyabiashara na wawekezaji, huku akisisitiza kuwa kikao kazi kama hiki ni muhimu kwa Taasisi na Taifa na utekelezaji wa makubalino utazaa matunda zaidi kwa kuondoa kero na kuleta umoja katika kufanya kazi.
Kikao kazi baina ya BRELA na TMDA ambacho kitahitimishwa Machi 1, 2024, kinatarajiwa kubaini na kuainisha maeneo ya ushirikiano ambayo yatasaidia katika kuandaa hati ya makubaliano ya ushirikiano (MoU) baina ya Taasisi hizi mbili. Ikumbukwe kuwa hivi karibuni kilifanyika kikao kazi kama hiki jijini Arusha kati ya BRELA na TPHPA ambapo walijadili na kufanya mashauriano ambayo yatarasimishwa na Hati ya Makubaliano (MoU) ambayo imepangwa kusainiwa hivi karibuni.
More Stories
Simbachawene:Waombaji wa ajira jiungeni na Mfumo wa Ajira Portal
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki