February 24, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kikwete: Rais Samia ni kiongozi shupavu

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

RAIS Mstaafu Jakaya Kikwete, amesema anachoonesha Rais Samia Suluhu Hassan katika kipindi hiki cha kero za umeme, maji na sukari, kinadhihirisha ushupavu wake katika uongozi.

Aidha, Kikwete ameenda mbali zaidi akisema; ” Changamoto ni sehemu ya uongozi na utulivu wake unawafanya wananchi pia kuwa watulivu. Na  ameendelea kuwa imara anapoendelea kutafuta suluhisho la changamoto hizo kwa kuwa ni mambo ya kawaida kwenye uongozi.”  

Kikwete ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam (UDSM) wakati wa utiaji saini mikataba sita ya ujenzi wa majengo 21 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ikiwa ni upanuzi na ujenzi wa kampasi mpya katika mikoa ya Lindi, Kagera, Zanzibar na Dar es Salaam.

Kikwete ambaye ndiye Mkuu wa Chuo cha UDSM ametoa kauli hiyo wakati akitoa shukrani kwa Serikali ambapo hafla hiyo ilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Elimu, Omari Kipanga.

Kiongozi huyo mstaafu amepongeza jitihada zinazofanywa na Rais Samia katika kuiletea nchi maendeleo, akisisitiza;  

“Tunamshukuru Rais Samia kwa uongozi wake tunaona mambo yanaenda vizuri, changamoto ni sehemu ya maisha, kungekuwa hakuna changamoto isingekuwapo haja ya kuwa na viongozi.

Changamoto hazitaisha, hata katika mataifa makubwa kama Marekani walipata uhuru 1,774 hadi leo hawajamaliza changamoto,” alisema.  

Kikwete amezidi kuhoji; “Sasa kweli tunatarajia Tanzania hii kutakuwa hakuna changamoto kabisa? Mara umeme, mara sukari wote tumepitia hayo utasikia kuna hiki mara kile mara kuna EPA hizo zote ni changamoto za uongozi. Uongozi haupoi kama ugali.

Uzuri ni kwamba changamoto zinatokea lakini Rais anaonesha uongozi wenye utulivu katika kukabiliana nazo. Zikitokea changamoto halafu kiongozi ana-panic, wananchi wana-panic zaidi,” alisema Kikwete.

Kuhusu upanuzi na ujenzi wa kampasi mpya za Chuo Kikuu ha Dar es Salaam, amesema ni utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) ambao chuo hicho kimepata Dola za Marekani 47 milioni (Sh110 bilioni).

“Nimekuwa nikiufuatilia mradi huu kwa ukaribu na maeneo yote tunayotakiwa kujenga nimeshafika, imechukua muda kidogo kuanza ujenzi kwa sababu kulikuwa na changamoto ambazo tumeshazitatua sasa tunaenda kuanza, hivyo niwasihi makandarasi kuzingatia muda na ubora,” amesema na kuongeza;

“Ucheleweshaji huo ulisababisha maneno kidogo, mfano siku moja nikiwa kule Lindi na mashemeji zangu wakasema wanasikia unafanyika mpango chuo kisijengwe hapa nikawaambia acheni uongo, maana maradhi ya Watanzania ni uongo.

Sijui hiki kirusi tumekipata wapi. Yaani wanaweza kutunga habari ya uongo halafu wakaieneza na wakati mwingine wakataka kuwahukumu watu kwa uongo waliouanzisha.”

Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa, William Anangisye amesema utekelezaji wa mradi wa HEET unafanyika sambamba na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025, na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (2020-2025).

Profesa Anangisye amesema kwa pamoja vinalenga kuimarisha uchumi wa viwanda ili kuendana na uchumi wa kati, na kuongeza fursa za ajira kwa makundi mbalimbali, hususan vijana.

“Sisi tunajiona kuwa na bahati kubwa kufikiwa na mradi huu kwani unarandana na dira yetu ya Udsm ‘Vision 2061’ na mpango mkakati wa chuo 2020/21-2024/25 vinavyolenga kufanya mageuzi ya kitaasisi yanayoendana na vipaumbele na mahitaji ya Taifa ya sasa na baadaye,” amesema.