Ni wa kampuni binafsi, walipewa kuzipeleka makao makuu ya benki, wakaingia mitini, Polisi yanasa watuhumiwa 32 yaokoa zaidi ya bilioni moja
Na Mwandishi Wetu
POLISI Kanda Maalum ya Dar es Salaam wanawashikilia watu 32 kwa tuhuma za wizi wa fedha zaidi ya sh. bilioni 2 mali ya Benki ya NMB.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema tukio hilo lilitokea Juni 8, mwaka huu saa tisa mchana katika Benki ya NMB tawi la Mbezi Beach.
Amesema katika tukio hilo wafanyakazi watano wa Kampuni ya Ulinzi ya Security Group of Africa @ SGA-Security Tanzania Limited wakiwa na gari namba T 853 DPX MITSUBISH CANTER walikabidhiwa kiasi cha fedha sh. 2 ,082,000,000 kwa maelekezo ya kuzisafirisha kutoka NMB Tawi la Mbezi Beach ili wazipeleke tawi la NMB Benki House Posta Mpya.
Amesema mara baada ya kukabidhiwa fedha hizo wafanyakazi hao badala ya kuzipeleka walipoelekezwa, walitoweka na fedha hizo.
“Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam kupitia kikosi kazi chake cha kupambana na ujambazi siku hiyo saa 12 jioni lilibaini kutelekezwa kwa gari hilo maeneo ya Mbagalarangi Tatu jirani na shule ya Saint, hivyo walianza ufuatiliaji,” amesema.
“Mara tu kikosi hicho kilipofatilia na kufika eneo lilipoonekana gari hilo na kubaini kuwa wafanyakazi hao watano wamekula njama na kuiba kiasi cha fedha sh.780,000,000 kutoka kwenye sanduku moja la chuma kati ya masanduku manne waliyokabidhiwa,” amesema
Aidha, amesema masanduku matatu yaliyokutwa katika gari hilo yalifunguliwa na kukutwa na kiasi cha fedha sh 1,302,000,000 na ndani ya gari hilo zilikutwa silaha mbili aina ya Short gun Pump Action yenye risasi 12 na Short gun Protector yenye risasi 5, pamoja na sare za kampuni hiyo.
Amesema watuhumiwa hao walikamatwa mkoani Mbeya na Kigoma wakiwa wamenunua vitu mbalimbali.
Alitaja vitu hivyo kuwa ni trekta Power Tiller aina ya TRA-Change Model 7C/15 lenye thamani ya Tsh 20,000,000, pikipiki moja aina ya SANLG ,TV flat screen moja aina SUNDA na vitu mbalimbali vya matumizi ya ndani kama kitanda, godoro, jiko la gesi,makochi .
Amesema mpaka sasa katika shauri hilo jumla ya sh 1,497,680,000, zimeokolewa, mbali na thamani ya vitu vilivyonunuliwa kutoka sehemu ya fedha zilizoibiwa.
“Jumla ya watuhumiwa 32 wamekamatwa na kuendelea kuhojiwa juu ya ushiriki wao kuhusiana na tukio hili na Jeshi letu linaendelea na msako mkali ili kuwakamata watuhumiwa wote waliohusika na tukio hili,” amesema.
More Stories
Maghorofa Kariakoo mikononi mwa Tume
ITA chatakiwa kutoa mafunzo ya viwango vya juu na kasi ya maendeleo ya Kisayansi
Wagombea CHADEMA wakipewa ridhaa,watakuwa wawazi