November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watoa rushwa uchaguzi serikali za mitaa kukiona cha moto

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Tabora imetoa onyo kwa wale wote wanaotarajia kugombea nafasi mbalimbali katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu kutojihusisha na vitendo vya rushwa.

Onyo hilo limetolewa jana na Mkuu wa TAKUKURU Mkoani hapa Mussa Chaulo alipokuwa akitoa taarifa ya utendaji kazi kwa vyombo vya habari na kubainisha mikakati ya Taasisi hiyo.

Amesema kuwa moja ya mikakati ya taasisi hiyo kwa mwaka huu kuelekea kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni kudhibiti vitendo vya rushwa ambapo watahakikisha elimu ya kutosha inatolewa mapema kwa wananchi wote.

Amefafanua kuwa elimu hiyo itawapa uelewa wa masuala ya rushwa ili watakapoona mgombea yeyote akitoa rushwa watoe taarifa haraka kwa Maafisa wa TAKUKURU ili wakamatwe na uchunguzi ufanyike, atakayethibitika kujihusisha na vitendo hivyo atachukuliwa hatua.

Chaulo ameongeza kuwa malalamiko yoyote yenye mlengo wa rushwa yatakayotolewa na wananchi au wagombea kabla, wakati na baada ya uchaguzi yatafanyiwa uchunguzi na hatua stahiki kuchukuliwa.

Ametoa wito kwa wakazi wa Mkoa huo na Watanzania wote kuendelea kutoa ushirikiano kwa Taasisi hiyo ili kuhakikisha vitendo vya aina yoyote ile vya kuomba au kupokea rushwa vinadhibitiwa katika nyanja zote ikiwemo miradi ya maendeleo.

Amebainisha kuwa licha ya vitendo hivyo kurudisha nyuma maendeleo ya jamii pia vinaweza kufanya wananchi wasipate Kiongozi bora anayeweza kusimamia maendeleo yao na taifa kwa ujumla.

Kamanda Chaulo amesisitiza kuwa TAKUKURU Mkoani Tabora itaendelea kutekeleza majukumu yake kama yalivyoainishwa katika sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007.

Aidha ameeleza kuwa wataendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha vitendo vya aina yoyote vya kuomba au kupokea rushwa havijitokezi katika jamii.