*Ni Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF
*Ahahidi ushirikiano, kulipa Pensheni kwa wakati,ukamilifu na usahihi
Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dodoma
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu; Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mha. Cyprian Luhemeja amezitaka taasisi zote zilizo chini ya ofisi hiyo kuhakikisha zinatoa elimu juu ya kazi wanazofanya ili Wananchi waweze kuelewa majukumu yao vyema kwa la kupatiwa huduma.Mha. Luhemeja amesema hayo Februari 20, 2024 katika kikao maalum cha kumtambulisha na kumkaribisha Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma(PSSSF), Bw. Abdul-Razaq Badru kufuatia kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungani wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kuingoza PSSSF.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu; Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mha. Cyprian Luhemeja, akihutubia wakati wa kumtambulisha Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF kwa watendaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu(Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu)
“Elimu juu ya taasisi zetu zote itolewe, haswa elimu ya Hifadhi ya Jamii iende kwa nguvu kwa wadau, naamini elimu ya Hifadhi ya Jamii ikieleweka vyema watu wengi hawatapoteza muda kwenye uwekezaji usio na tija” alisema Mha. Luhemeja.
Akimkaribisha Bw. Badru, Mha. Luhemeja alisema, “Ndugu zangu naomba muungane nami kumkaribisha Bw. Badru ambaye ameteuliwa hivi karibuni kuongoza PSSSF, naomba tumpatie ushirikiano ili aweze kutekeleza vyema majukumu yake, Bw. Badru hii ndio timu yako sasa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, karibuni sana”.
Mha. Lumemeja alifurahiswa na kauli ya Bw. Badru kuwa mwelekeo wa utendaji lazima uendane na kusudio na lengo la uwepo wa taasisi husika.
“Kweli nimefurahishwa na hoja ya Bw. Badru, kwamba ili utendaji kazi uende vyema ni lazima mwelekeo ulenge kusudio na lengo la taasisi husika, hivyo kila mmoja wetu ni lazima ajue mwelekeo wa taasisi yake ili aweze kufikia malengo” alifafanua Mha. Luhemeja.
Kwa upande wake, Bw. Badru alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kumwamini na kumteua kuwa Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF,ameahidi utendaji bora kwa kuzingatia miongozo na kanuni zilizopo.
Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Bw. Abdul-Razaq Badru akizungumza baada ya kutambulishwa kwa kwa watendaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu)
“Kwa kweli nashukuru kwa kuwa sehemu ya timu hii chini ya ofisi ya Waziri Mkuu, ninahidi ushirikiano kwenu ili kwa pamoja tuweze kutekeleza vyema majumu yetu” alisema Bw. Badru.
Bw. Badru alisema, PSSSF imejipanga kutekeleza vyema majukumu yake na kuendelea kutoa huduma bora kwa Wanachama kwa kuendelea kutumia TEHAMA ili kila mwanachama afikiwe kwa wakati.
“Tutaendelea kutoa elimu mahususi kwa Wanachama ili waelewe zaidi juu ya PSSSF, tunahakikisha kila mdau atafikiwa na tunaahidi kulipa pensheni kwa wakati, ukamilifu na usahihi” aliahidi Bw. Badru
Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Bw. Abdul-Razaq Badru(kushoto) akiwa pamoja na Bw.John Mduma Mkurugenzi Mkuu wa WCF na Bi. Khadija Mwenda, Mtendaji Mkuu wa OSHA wakifatilia hotuba iliyotolewa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu; Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mha. Cyprian Luhemeja, wakati akimtambulisha Bw. Badru.
Rais wa Jamhuri ya Muungani wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Februari 6, 2024 alimteua Bw. Badru kuwa Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF.
More Stories
Asilimia 64.35,ya wafanyabiashara wabainika kutokuwa na leseni
UAUT wajipanga kuzalisha wanafunzi waliopikwa vizuri
Wanafunzi 7176, kufanya mtihani wa taifa