November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ujenzi wa kivuko waunganisha mtaa wa Kilimani na Tulieni

Na George Mwigulu, Timesmajiraonline,  Mpanda.

Imeelezwa kuwa kukamilika kwa ujenzi wa kivuko katika Mto Nsemlwa Manispaa ya Mpanda, kilichokuwa kinasababisha mafuriko utasaidia kuwaunganisha wananchi wa mtaa wa kilimani na Tulieni.

Hayo yamesemwa leo,Februari 15,2024 na Diwani wa Kata ya Nsemlwa,Bakari Kapona wakati akimpongeza mdau wa maendeleo Mkoa wa Katavi,Mhadisi Ismail Nassoro ambaye ndiyo aliyejenga kivuko hicho chenye thamani ya shilingi milioni 11.6.

Kapona amesema kuwa kitendi alichokifanya Mhandisi huyo ni kumuunga mkono Rais Dkt.Samia Suluhu Hassain kwa kazi anayoifanya ya ujenzi wa miradi ya maendeleo.

Ameeleza kuwa wakati ambao mvua zinaendelea kunyesha kwa wingi kunauharibifu mkubwa wa miundombinu ya barabara na mito kujaa maji na kuwa kero inayohatarisha maisha yao na kushindwa kufanya kazi za maendeleo.

Amesema kuwa miundombinu ya barabara ni muhimu kuendelea kuwa imara na pindi inapoharibika ni muhimu wadau mbalimbali kujitokeza kushirikiana na mamlaka husika ya TARURA kutegeneza miundombinu hiyo kwa faida ya jamii.

“Kama mwakilishi wa wananchi kazi iliyofanyika ni kubwa ya kizalendo kwa kuwa inatoa faraja kwa wananchi kwa mazingira ambayo awali yaliyokuwepo mtoni hapo ni hatari kwa usalama wa jamii,”amesema.

Baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Mpanda wakizungumza kwa wakati tofauti wameeleza kivuko hicho kitapunguza muda wa kusafiri,kuboresha chaguo za usafiri na kutoa ufikiaji wa maeneo ambayo hapo awali hayakuweza kufikiwa.

Rhoda Emmanuel,Mkazi wa Mtaa wa Kilimani amesema wakati wa mvua mto huo hujaa maji na kuwalizimu kutumia fedha kulipa watu wa kuwavusha ambapo kwa wananchi wasiokuwa na fedha hushindwa kuvuka na kukwamisha shughuli zao.

Ameiomba serikali kupitia mamlaka zinazohusika kuunga mkono juhudi zinazofanywa na wadau wa maendeleo kwa kushirikiana nao ili kuhakikisha miundombinu ya barabara inaimalika na kudumu muda mrefu.

Baraka Daudi mmoja wa wananchi wa mtaa wa Tulieni ameeleza kuwa wakati wa mvua nyingi kunyesha miundombinu mingi ya barabara imeharibika na kuwa ngumu kuvukaa kutoka eneo moja na jingine ambapo kitendo cha wananchi wazalendo kujitokeza kuisaidia serikali kujenga miundombinu hiyo kisitafsiriwe kisiasa bali kizalendo na utaifa.

“Ujenzi wa kivuko hiki utafungua shughuli za kiuchumi hususani katika maeneo yetu haya ya mtaa ya Kilimani na Tulieni huku ndiko wananchi wenye kipato cha chini hufanya biashara zao za mbogamboga,mkaa na mahindi ya kuchemsha hivyo kukamilika ujenzi huo utagusa mwiligiliano wa kibiashara,”amesema Daudi.

Mhadisi Ismail Nassoro, Mdau wa maendeleo Mkoa wa Katavi amesema ameguswa na kero ambayo wananchi pamoja na wananfunzi waliokuwa wakipata ya kushindwa kupita kwenye eneo hilo kwenda shule na wananchi kwenda kufanya shughuli zao za kiuchumi.

Nassoro amesema kiasi cha fedha Mil 11.6 zimetumika kwenye ujenzi huo ambapo ubora wa ujenzi ulikuwa kipaumbele ili kuwezesha watembea kwa miguu kupita bila wasiwasi na usafiri wa magari madogo na pikipiki kupita.