Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
WAJUMBE wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira wameagiza kuharakishwa utekelezaji mradi wa Maji wa Miji 28 Mkoani Tabora ili kufikisha huduma ya maji safi kwa wakazi wa Wilaya 3 za Sikonge, Urambo na Kaliua.
Wametoa agizo hilo juzi walipotembelea mradi huo ili kujionea kasi ya utekelezwaji wake kwa lengo la kumaliza kilio cha wananchi wanaoishi katika vijiji mbalimbali wilaya humo.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Kalenga, Jackson Kiswaga alisema kuwa mradi huo ni muhimu sana kwa ustawi wa jamii katika wilaya hizo, hivyo akaomba uharakishwe ili kuwaondolea kero ya kukosa maji.
Amesisitiza kuwa mradi huo wa kimkakati unaogharimu zaidi ya sh bil 145 ni wa muhimu sana kwa wakazi wa wilaya hizo hivyo akamwagiza Mkuu wa Mkoa kufuatilia kwa karibu zaidi utekelezwaji wake ili ukamilike kwa wakati.
Aidha ameagiza Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Tabora (TUWASA) kusimamia ipasavyo mradi huo na kama kuna changamoto yoyote itatuliwe haraka ili kutokwamisha utekelezaji wake.
Mhesh.Kiswaga amempongeza Waziri wa Maji, Naibu wake na Katibu Mkuu kwa kusimamia vyema utekelezaji miradi ya maji katika maeneo mbalimbali, aliwataka kuweka mikakati mizuri ya usambazaji maji ya visima katika maeneo mengi zaidi.
Mjumbe wa Kamati hiyo Asya Mohamed ameshauri Wizara hiyo kuwapa mafunzo zaidi Wataalamu wake ili kuwapa mbinu mpya za utekelezaji miradi ya maji ikiwemo matumizi ya vifaa vya kisasa vya kubaini uwepo wa maji ardhini.
Aidha ameshauri suala la uvunaji maji ya mvua kuwekewa msisitizo mkubwa ikiwemo wananchi kuelimishwa namna ya kuvuna maji hayo ili kuongeza upatikanaji maji miongoni mwa jamii.
Wabunge wengine Rita Kabati, Soud Mohamed na Kavejuru Felix wameshauri TUWASA na Wizara ya Maji kuangalia namna ya kupanua Bwawa la Maji la Igombe ili kuongeza ukubwa wake na maji hayo kusambazwa katika mikoa jirani.
Mbunge Agness Hokororo na Mhandisi Stella Manyanya walishauri vijiji vyote ambavyo havitafikiwa na Mradi wa Maji wa Miji 28 kuwekewa mkakati wa kupelekewa huduma ya maji safi na salama ili kumtua mama ndoo kichwani.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi ameahidi kufanyia kazi ushauri na mapendekezo yote yaliyotolewa na Wajumbe wa Kamati hiyo ili kuboresha utendaji wa Wataalamu wa Wizara hiyo.
Amesisitiza kuwa watahakikisha Mradi wa Maji wa Miji 28 unaotekelezwa katika wilaya 3 za Mkoa huo unakamilika kwa wakati na kwa kiwango kinachotakiwa ili kutimiza azma ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo kichwani.
More Stories
5 “best” Bitcoin Online slots games
Best Web based casinos Norway Your own #1 Norwegian Online casinos 2024
Prof. Mwakalila asisitiza uadilifu, uzalendo kwa wanafunzi wapya chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere