January 1, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tengeni bajeti kuanzisha madarasa mubashara – Mchengerwa

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Miko na Serikali za Mitaa, Mohamed Mchengerwa amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri kutenga kwenye bajeti ya mwaka 2024/25 fedha za kutosha kununua vifaa vya TEHAMA.

Hatua hii ni kuwezesha uanzishwaji wa madarasa janja yatakayotumika ufundishaji mubashara ikiwa ni njia ya kukabiliana na uhaba wa walimu na kuongeza maarifa kwa wanafunzi.

Mchengerwa ametoa maagizo hayo mara baada ya kuzindua na kushuhudisha majaribio ya ufundishaji mubashara kati ya Shule ya Sekondari Kibaha Mkoa wa Pwani na Shule ya Sekondari Dodoma mkoani Dodoma.

Alisema pamoja na agizo lake la kutaka kufanyika msawazo wa walimu bado kumekuwapo na uhaba wa walimu katika ngazi zote za elimu ya awali, misingi upatao 271,028 na kuwa uanzishwaji wa ufundishaji mubashara utasaidia kukabiliana na changamoto hiyo.

“Nilitoa maelekezo ya kufanyika kwa msawazo wa walimu katika maeneo mbalimbali, lakini bado kuna uhaba mkubwa wa walimu katika ngazi ya elimu ya awali, msingi na sekondari, mpaka muda huu nimesimama hapa nazungunza uhaba ni walimu 271,028 ambao walipaswa kuwa kwenye shule zetu na ndio maana tumekuja na teknolojia hii ya elimu mubashara.”

Kwa upande wa elimu ya awali na msingi uhaba ni walimu 186,385 na kwa sekondari ni 84,643.

Alisema ufundishaji mubashara ni moja ya jitihada za serikali ya awamu ya sita chini ya ugongozi wa Rais Samia, Suluhu Hassan wa kwenda kupunguza uhaba wa walimu nchini.

“Kwa kuwa sasa tunakwenda kwenye majaribio ya TEHAMA ya ufundishaji mubashara, tunatambua yatakuwa na changamoto mbalimbali na changamoto ya kwanza ni uhaba wa vifaa.”

“”Niwaelekeze wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kuhakikisha wanatenga kwenye bajeti ijayo ya 2024/25 wanatenga fedha za kutosha ili tuanze mchakato wa kununua vifaa hivi vya TEHAMA.”

Alisema ufundishaji mubashara utasaidia katika kupunguza changamoto ya uhaba wa walimu na kuongeza ufahamu na maarifa kwa wanafunzi wanaosoma katika shule mbalimbali katika ngazi ya awali, msingi na sekondari.
Mchengerwa alisema jitihada za serikali kuhakikisha tunakwenda kupunguza uhaba wa walimu na moja ya njia ya kupunguza uhaba wa walimu ni kwenda kufanya msawazo katika maeneo ambayo kuna walimu wengi

Lakini tukagundua kuwa pamoja na msawazo huu bado uhaba wa walimu utaendelea kuwepo na ndio sasa tumekuja na mfumo huu wa Tehama ambao ni wa ufundishaji Mubashara.

Nimejioena na nimeridhika kwa majaribio haya ya ufundishaji mubashara ambayo tumeanza nayo kwa jitihada hizi

Aidha, Mchengerwa amewaagiza wakuu wa mikoa na makatibu tawala wa mikoa kuteua shule maalumu ambayo itakuwa nguzo ya kusambaza mifumo hii ya TEHAMA katika shule mbalimbali katika maeneo yao.
“Katika mkoa lazima wateue shule kama walivyofanya hapa Dodoma, na kwa Mkoa wa Pwani kama walivyofanya kule Kibaha, na wakuu wa mikoa mingine waanze kuteua shule moja ambayo itakuwa nguzo katika shule mikoa husika kwenda kulitekeleza mara moja.”

Mchengerwa pia amemuagia Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI kushirikiana na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknlojia kwenda kutekeleza programu hiyo ili ienee nchi nzima.
Alisema mpango wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI ni kubakikisha ifikapo Desemba 2025 ufundishaji mubashara uwe umeenea nchi nzima.

“Tunajua kuenea kwa programu kutasaidia vijana wetu watapa elimu iliyo sawa na watapata mafunzo kwa walimu walioandaliwa vizuri. Hivyo endeleeni kufanya mapinduzi makubwa ya TEHAMA ambayo yataleta usawa na tija kwa wanafunzi wote wanaosoma elimu ya awali, msingi na sekondari.”

Aidha, Mchengerwa alisema wakati Ofisi ya Rais-TAMISEMI wanakwenda kutekeleza suala la msawazo wa walimu mashuleni, inakuja na mkakati ya kuwafanya walimu waliohitimu shahada au diploma ya ualimu kufundisha katika shule za serikali kwa muda wa miezi sita au mwaka mmoja kwenye shule mbalimbali hasa kwenye maeneo wanayotoka.

“Tukiweza kukitekeleza hili kwa kushirikiana na wizara ya elimu tutaweza kukabiliana na uhaba wa walimu hasa katika shule zenye uhaba mkubwa na hii pia tutawapa fursa za ajira pale zinapotangazwa.”

Naye Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI anayeshughulikia elimu, Dk Charles Msode alisema uwekaji wa darasa janja kwenye maeneo mablimbali watoto wanaweza kusoma kwa kufundishwa na mwalimu mmoja.
“Mfano mwalimu wa fizikia aliyeko Kibaha anaweza kufundisha shule zozote zilizo na darasa janja, hivyi hata mtoto.

Mwalimu wa Shule ya Sekondari Laurian Nyoni kwa mfumo huo utasaidia katika ufundishaji hasa kutokana na kuwa walimu kuhitajika zana za kufundishia na unaongeza hamasa kwa wanafunzi kujifunza.

Pia itasaidia kubadilishana uzoefu hasa kutokana na kuwa kila mwalimu hawezi kuwa mahiri mada zote za somo lake.

Kwa upande wa mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya sekondari Dodoma, Fauzia Said alisema mfumo huo umewasaidia kuongeza uelewa kwa kupata maarifa kutoka kwa walimu mbalimbali.

Naye Ephraem Mbuyi alisema:” nimejisikia furaha kusoma pamoja na wenzetu wa Kibaha, tekinolojia hi inatusaidia kubadilisha maarifa na wenzetu, tunaishukuru sana serikali kwa hili na tunaomba waongeze kasi ili isaidie kuongeza wigo.”