November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TAWA yaunga mkono serikali sekta ya elimu

Na. Mwandishi wetu

Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Dkt. Vincent Mashinji amesema Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imeendelea kuunga mkono jitihada za Baba wa Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha elimu inakuwa kipaumbele wilayani Serengeti.

Dkt. Mashinji ameyasema hayo Jana wakati wa ziara ya kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na TAWA kwa kushirikiana na nguvu za wananchi kwa fedha zinazotokana na shughuli za uwindaji wa kitalii, ziara iliyofanywa na TAWA wilayani humo.

“TAWA moja kwa moja wameweza kugusa maisha ya wananchi katika jamii hasa katika masuala muhimu ambayo hata Baba wa Taifa aliyeanzisha haya Mapori aliyasisitiza, suala la elimu..” amesema na kuongeza

” Kwa kumuunga mkono Rais Samia , TAWA wameweza kutujengea miradi 6 ambayo imejielekeza katika Sekta ya elimu” ameongeza Dkt. Mashinji

Akibainisha miradi hiyo Mkuu huyo wa wilaya amesema katika Kata ya Sedeco, vijiji vya Bonchugu na Mbilikiri TAWA wamejenga chumba kimoja cha darasa huku Kata ya Kyambahi Kijiji cha Bokore wamejenga vyumba viwili vya madarasa.

Pia katika Kata ya Manchira Kijiji cha Kazi TAWA wamejenga nyumba moja (1) ya Mwalimu na matundu kumi ya vyoo katika shule ya Msingi Rwamchanga kikiwemo choo kwa ajili ya watu wenye changamoto ya viungo vya mwili (walemavu) pamoja na chumba maalumu cha wanafunzi wakike kwa ajili ya kubadilishia taulo.

Aidha ameushukuru uongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Menejimenti ya TAWA kwa kurejesha rasilimali ambayo ni endelevu na kuhakikisha kile kidogo kinachopatikana katika uhifadhi kinarudi mikononi mwa wananchi.

Kwa niaba ya wananchi, Diwani wa Kata ya Kyambahi Herman Kinyalire amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia TAWA kwa kuwezesha ukamilishwaji wa miradi mikubwa minne katika Kata yake ambayo ni madarasa manne , vyumba viwili vya madarasa pamoja na thamani za shule.

Aidha amesema utekelezaji wa miradi hiyo umechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza ujangili katika Kata yake na kuwafanya wananchi waongeze ushirikiano katika uhifadhi wa wanyamapori kwa kuwa wanaziona faida za moja kwa moja zinazotokana na shughuli za uhifadhi.

Kwa upande wake Afisa Habari wa TAWA Beatus Maganja amesema TAWA haiwezi kuongelea mafanikio wanayoyapata ikiwa ni pamoja utekelezaji wa miradi hiyo bila kuhusisha Jitahada za dhati zilizofanywa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipocheza Filamu Maarufu ya Tanzania The Royal Tour ambayo imekuwa chachu ya ongezeko la watalii wa Uwindaji katika hifadhi mbalimbali zinazosimamiwa na Taasisi hiyo.

Maganja amesema TAWA imekuwa miongoni mwa Taasisi zilizonufaika na matokeo ya filamu hiyo ambapo katika miezi 10 ya awali kwa Mwaka wa fedha 2022/23 TAWA ilirekodi ongezeko la idadi ya watalii kutoka 541 mpaka 692 idadi ambayo ilivunja rekodi.