December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Polisi yawatambua waliotoa huduma bora kwa wananchi Arusha

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online, Arusha

Jeshi la Polisi Mkoani Arusha katika kuhakikisha linaboresha huduma bora kwa Wananchi limeendelea kuwatambua na kuwapongeza Askari wa Jeshi hilo wanaofanya kazi vizuri zaidi ya kuhudumia wananchi Mkoani humo.

Akitoa vyeti vya Pongezi kwa Askari hao katika siku ya ‘Police Day’ leo Januari 26, 2024 katika viwanja vya Polisi Arusha, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Justine Masejo amesema Jeshi hilo limekua na utaratibu wa kuwatambua na kuwapongeza Askari wanaofanya kazi vizuri zaidi kila mwaka.

ACP Masejo ameongeza kuwa Jeshi hilo litaendelea kuwatambua na kuwapongeza Maafisa, Wakaguzi na Askari watakaofanya kazi vizuri ya kutoa huduma bora ikiwa ni pamoja na kubaini na kutanzua uhalifu ikizingatiwa kuwa Mkoa huo ambao ni kitovu cha utalii hapa nchini.

Halikadhalika amewataka Askari wengine kuiga mfano mzuri kutoka kutoka kwa askari waliopata vyeti vya sifa na zawadi lakini pia kuongeza juhudi katika utendaji wao wa kazi ili Mkoa huo uendelee kuwa shwari na wananchi waendelee na shughuli zao za kiuchumi kwa amani.

Sambamba na hilo amewataka Askari kuhakikisha wanaimarisha usalama kwa wananchi lakini pia kushirikiana nao ili kutimiza azma ya Jeshi hilo ya kushirikisha wananchi katika kuzuia uhalifu hasa kwa kuzingatia mkoa huo ni kitovu cha utalii Nchini lakini pia mikutano mbalimbali ya kimataifa hufanyika.

Nao baadhi ya Askari waliopata vyeti vya sifa na zawadi pamoja na kushukuru jeshi hilo kwa kuwatambua kwa utendaji wao wa kazi, wamebainisha kuwa zawadi hizo zimetokana na ushirikiano mzuri toka kwa Askari wengine pamoja na wananchi ambao wamekua wakishirikiana nao katika kuzuia uhalifu huku wakisema zawadi hizo zitaongeza ufanisi katika utendaji wao wa kazi.