November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Utajiri wa Mo Dewji wapaa, Afrika Mashariki akamatiki *Aendelea kuwa bilionea mwenye umri mdogo zaidi kwa miaka 10 mfululizo

Na Mwanjiri Wetu, TimesmajiraOnline,Dar

THAMANI ya utajiri wa mfanyabiashara wa Kitanzania, Mohammed Dewji imepanda kutoka dola za Marekani bilioni 1.5 mwaka jana hadi kufikia dola bilioni 1.8, mwaka huu, hiyo ni kwa mujibu wa Jarida la Forbes la hivi punde.

Katika orodha ya Forbes ya mabilionea wenye utajiri mkubwa Barani Afrika, ni pamoja na Mo Dewji ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji Mohammed Enterprise Tanzania Ltd (MeTL).

Mo Dewj amepanda kwa utajili mwaka huu kutoka nafasi ya 13 aliyokuwa akishikilia mwaka jana hadi nafasi ya 12.

Katika orodha hiyo, Mo Dewji anaendelea kuwa bilionea mwenye umri mdogo zaidi kwa miaka 10 mfululizo, akiwa na umri wa miaka 48 na ndiye bilionea pekee Afrika Mashariki aliyeonekana kwenye orodha hiyo iliyochapishwa Forbes .

Kulingana na Forbes, METL inaajiri watu 40,000 kwenye nchi za Afrika Mashariki na Kati kutoka watu 35,000 wa mwaka jana.

METL inafanya kazi katika utengenezaji wa nguo, kusaga unga, vinywaji na mafuta ya kula katika Afrika Mashariki, Kusini na Kati.

Mbali na Tanzania, METL inafanya kazi katika nchi 10 za Afrika zikiwemo Uganda, Ethiopia na Kenya.

Mo Dewji, ni bilionea pekee wa Tanzania, aliyetoa ahadi mwaka 2016, akiahidi kutoa angalau nusu ya utajiri wake kwa ajili ya misaada.

Katika mabilionea 20 kwenye orodha ya Forbes ya mwaka huu, utajiri wa matajiri wa Afrika una thamani ya dola bilioni 82.4 kwa pamoja. Hiyo ni dola milioni 900 kutoka dola bilioni 81.5 za mwaka jana.

Mbali na Mo Dewji, Jarida la Forbes limewataja matajiri wa Afrika na utajiri wao kwenye mabano kuwa ni pamoja na Aliko Dangote ($13.9bn), Johann Rupert & family ($10.1bn), Nicky Oppenheimer & family ($9.4bn), Nassef Sawiris ($8.7bn), Mike Adenuga ($6.9bn), Abdulsamad Rabiu ($5.9bn) , Naguib Sawiris ($3.8bn), Mohamed Mansour ($3.2bn), Koos Bekker ($2.7bn), Patrice Motsepe ($2.7bn), Issad Rebrab & family ($2.5bn), na Strive Masiyiwa ($1.8bn).

Wengine ni Aziz Akhannouch & family ($1.7bn), Othman Benjelloun & family ($1.4bn), Youssef Mansour ($1.3bn), Yasseen Mansour ($1.2bn), Christoffel Wiese ($1.2bn), Michiel Le Roux ($1.1bn) na Femi Otedola ($1.1bn).

Bara la Afrika linasalia kuwa mojawapo ya maeneo magumu zaidi duniani kujenga na kushikilia – utajiri wa dola bilioni, kama wawekezaji wa kimataifa wanaendelea kuhangaika na masoko yake ya hisa.

Biashara inajitahidi dhidi ya uchumi mbaya, miundombinu duni na viwango vya kubadilisha fedha Mwaka 2023 misukosuko pia ilifanya hisa za Kiafrika zisiwe na mvuto kwa wawekezaji wa kigeni.