Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
KUTEKELEZWA kwa kiwango kikubwa miradi ya elimu, afya, maji na miundombinu ya barabara katika halmashauri ya manispaa Tabora kumefanikiwa kupunguza kero ya upatikanaji huduma mbalimbali za kijamii hivyo kufanikisha utekelezaji ilani ya uchaguzi kwa asilimia 100.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Seif Salum Seif alipokuwa akiongea na gazeti hili ofisi kwake ambapo alibainisha kuwa miradi yote imetekelezwa kwa ufanisi mkubwa na kuwezesha wananchi kunufaika.
Alisema kwa mwaka jana na mwaka huu pekee kiasi cha sh bil 41.4 zilizotolewa na serikali ya ya awamu ya 6 chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kimewezesha kuboreshwa huduma za kijamii katika sekta mbalimbali.
Alibainisha kuwa fedha hizo zimeleta tija kubwa katika utoaji huduma za afya na nyinginezo kuanzia kwa watalaamu na jamii kwa ujumla huku zikichochea kuongezeka kwa kiwango cha ufaulu wa wanafunzi katika shule zote.
Mbali na sekta za elimu na afya Seif alibainisha sekta zingine zilizoboreshwa kwa kiasi kikubwa katika halmashauri hiyo kuwa ni maji, kilimo, miundombinu ya barabara na utawala ambapo wameweza kujenga nyumba bora za watumishi na kutoa usafiri kwa watendaji wa vijiji na kata ili kuwarahisishia usafiri.
Akifafanua zaidi alisema mafanikio hayo yameweza manispaa kutekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM kwa asilimia 100 na kuongeza kuwa wataendelea kusimamia ipasavyo fedha zote zinazoletwa na serikali kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.
‘Tunamshukuru sana Rais Samia kutupatia fedha hizo, pia ametuongezea kiasi kingine cha sh bil 6.4 kwa ajili ya kuboreshwa huduma za afya katika hospitali yetu ya wilaya na kutupatia vifaa vya kisasa vya kutolea huduma hizo’, alisema.
Baadhi ya huduma zilizoboreshwa katika hospitali hiyo ni mama na mtoto ambapo sasa akinamama wajawazito kutoka katika zahanati na vituo vya afya mbalimbali watapata huduma bora zaidi.
Alitaja huduma nyingine kuwa ni ya mionzi (x-ray na ultra sound), ambayo imepunguza kero ya wananchi kufuata huduma hiyo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Kitete.
Seif aliongeza kuwa pia wamejenga vituo vya afya na zahanati katika kata na vijiji mbalimbali na zingine kuboreshwa miundombinu na zingine ziko katika hatua mbalimbali ya ukamilishaji ili kuwezesha wananchi kupata huduma bora.
Aidha alimshukuru Rais Samia kwa kuwapatia sh bil 8.2 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya, vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo na nyumba za walimu ili kuboresha mazingira ya kusomea watoto.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Ramadhan Kapela alisema kuwa wanajivunia mafanikio makubwa waliyopata katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023 na 2023/2024 na kuahidi kuwa halmashauri hiyo itaendelea kufanya makubwa zaidi kwa manufaa ya jamii.
Aliongeza pia kuwa wanajivunia kuboreshwa kwa miundombinu ya shule kongwe zote za sekondari zilizopo katika manispaa hiyo za Tabora wavulana, Tabora wasichana, Milambo na Kazima kwa gharama ya sh bil 17.7 na kubainisha kuwa shule zote katika manispaa hiyo sasa zina mwonekano wa kisasa.
More Stories
Ushiriki wa Rais Samia G20 wainufaisha Tanzania
Rais Samia apeleka Bil. 6 kuboresha sekta ya elimu Kaliua
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM