November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Madaktari bingwa JKCI kutoa matibabu ya moyo Tabora

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

MADAKTARI Bingwa na Wataalamu wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ya Jijini Dar es salaam wanatarajia kuwasili Mkoani Tabora mwezi huu kwa ajili ya kutoa huduma ya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa wakazi wa Mkoa huo na Mikoa jirani.

Huduma hizo za tiba mkoba zinazojulikana kwa jina la Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan Outreach Services zitatolewa katika viwanja vya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo Kitete kwa wananchi wote.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari jana Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa Taasisi hiyo Anna Nkinda amesema kuwa Wataalamu wa JKCI watatoa huduma hiyo kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo Kitete.

Amesema huduma ya upimaji wa magonjwa hayo itatolewa kwa watoto na watu wazima kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa huo na Mikoa jirani kuanza tarehe 15-19 Januari 2024 na itaanza majira ya saa 2.00 asubuhi hadi saa 10.00 jioni katika viwanja hivyo.

Anna ameeleza kuwa wote watakaogundulika kuwa na matatizo ya moyo watafanyiwa uchunguzi zaidi na kupatiwa matibabu hapo hapo au kupewa rufaa ya kwenda kutibiwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo Upanga Jijini Dar es salaam.

‘Hii ni fursa muhimu sana, tunaomba wananchi wajitokeze kwa wingi ili kupima afya zao, atakayegundulika kuwa na matatizo ya moyo ataanzishiwa matibabu mapema iwezekanavyo’, alisema.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Kitete, Dkt Mark Waziri amefafanua kuwa huduma ya upimaji na kumwona Daktari Bingwa itatolewa bure na bima za aina zote zitatumika na kwa wasio na bima watapata ushauri bure ila watakaohitaji kupimwa na dawa watachangia gharama kidogo.

Ameongeza kuwa msamaha utatolewa kwa makundi maalumu na pale itakapobidi huku akibainisha kuwa zoezi la utoaji huduma za kibingwa na bobezi za magonjwa ya moyo na mengineyo litafanywa kuwa endelevu kwa manufaa ya jamii na sio kwa faida.

Amebainisha kuwa kambi hiyo ya siku 5 itanufaisha wakazi wa Mkoa huo na Mikoa jirani ya Katavi, Kigoma, Singida na Shinyanga pamoja na ile ya Kanda ya Ziwa yaani Simiyu, Geita, Mwanza na Mara.

Amesisitiza kuwa huduma hii inabebwa na kauli mbiu ya JKCI isemayo ‘Afya ya Moyo Wako ni Jukumu Letu’.