Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Nzega
SERIKALI ya awamu ya 6 imemaliza utoro sugu na ufaulu duni wa wanafunzi wa shule ya msingi Mwandu iliyoko katika kata ya Mwasala Wilayani Nzega Mkoani Tabora baada ya kupeleka sh mil 361 ili kujengwa shule mpya katika kijiji jirani cha Mwandugwidako.
Hayo yamebainishwa juzi na Afisa Mipango wa halmashauri hiyo James Raymond alipokuwa akiongea na mwandishi wa gazeti hili.
Amesema ujenzi wa shule hiyo umeleta faraja kubwa kwa wakazi wa kata hiyo kwa kuwa watoto wengi walikuwa wanaacha shule kutokana na changamoto ya kutembea umbali mrefu ikiwemo kufurika kwa mto unaotenganisha wakazi wa vijiji 3 vya kata hiyo.
‘Shule hii imemaliza kilio cha muda mrefu cha wananchi kwani zaidi ya nusu ya watoto walikuwa hawamalizi darasa la 7 na hata wanaomaliza wengi wao walikuwa wanashindwa kuendelea na masomo ya sekondari,’ amesema.
Aliyekuwa Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Mwasala Jonas Kwiyera ambaye sasa ni Mkuu wa shule hiyo mpya ameeleza kuwa wastani wa watoto 50 hadi 100 walikuwa wanaacha shule kila mwaka kutokana na changamoto hizo.
Ametoa mfano wa watoto 320 walioanza darasa la kwanza mwaka 2017 shuleni hapo kuwa waliomaliza la saba ni 147 tu, hivyo akashauri kujengwa daraja pia litakalopunguza adha ya kuvuka mto wakati wa masika.
‘Tunamshukuru sana Rais wa awamu ya 6 Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutujengea shule mpya hususani katika Kijiji hiki cha Mwandugwidako kwa kuwa watoto wengi wanaotoka kijijini hapo ndio wanaongoza kwa kuacha shule,’ amebainisha.
Naye Afisa Elimu Sekondari wa wilaya hiyo Magesa Mgeta amefafanua kuwa kujengwa kwa shule hiyo ng’ambo ya mto na karibu na makazi ya wakazi wa kijiji cha Mwandugwidako kumewasogezea huduma ya elimu karibu zaidi hivyo utoro sugu na kuacha shule vitakoma.
Aidha amepongeza serikali kwa kujenga shule mpya ya sekondari katika kata hiyo kwa gharama ya sh mil 603 kwani watoto walilazimika kutembea umbali wa zaidi ya km 20 kwenda sekondari ya kata jirani ya Lusu hali iliyopelekea watoto wengi kushindwa kuendelea na masomo kutokana na umbali mrefu.
Ameeleza kuwa hali ilikuwa mbaya kwani kwa mwaka huu pekee kati ya watoto 187 walioanza kidato cha kwanza mwaka jana waliofanya mtihani wa kidato cha pili ni watoto 47 tu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Mhandisi Modest Apolinary amemshukuru Rais Samia kwa dhamira yake njema ya kumaliza kero za wananchi katika sekta zote katika halmashauri hiyo.
Amebainisha kuwa katika kipindi cha miaka 2 tu ya utawala wake miundombo ya shule zote za msingi na sekondari imeboreshwa kwa kiasi kikubwa sana ikiwemo kujengwa shule mpya katika maeneo yote yaliyokuwa hayafikiki ili kupunguza kero ya watoto kutembea umbali mrefu.
Aidha amempongeza kwa kuipatia halmashauri hiyo zaidi ya sh bil 2 kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya Halmashauri na sh bil 1 za ujenzi wa hospitali mpya ambayo inajengwa katika kijiji cha Lubisu kata ya Utwigu na inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu wa Desemba.
More Stories
Tanga kutumia vituo 5405,kupiga kura leo
NMB yatoa msaada wa vifaa Mufindi
Viongozi wa dini Katavi waomba wananchi kujitokeza kupiga kura