Na Moses Ng’wat, TimesMajira Online, Songwe.
WAMILIKI wa migodi kata ya Saza wilayani Songwe wametakiwa kutatua changamoto zinazowakabili waajiriwa wao ikiwa ni pamoja na kuwalipa stahiki zao kwa wakati ili kuepusha migogoro katika eneo hilo.
Hayo yamesemwa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Songwe Kamshna Msaidizi wa Polisi Theopista Mallya Disemba 11, 2023 alipofanya kikao na wachimbaji wadogowadogo wa madini na wamiliki wa migodi katika eneo hiyo lengo likiwa ni kusikiliza kero, changamoto na kupata ushauri kuhusiana na mambo ya ulinzi na usalama.
“Wamiliki wa migodi mmekuwa chanzo cha migogoro ambayo inapelekea kutokea kwa uhalifu na ukatili katika eneo hili kutokana na kutokutenda haki kwa waajiriwa wenu, walipeni mishahara hawa vijana kwani hao ndio wanafanya shughuli zenu za uchimbaji ziendelee pia wapeni mikataba yenye tija na acheni kuwatisha pindi wanapodai mishahara yao ili kuondoa migogoro katika eneo hili”. Amesema Kamanda Mallya
Kamanda Mallya alihitimisha kwa kuwataka viongozi wa eneo hilo kila mmoja kwenye nafasi yake kuwajibika na kutenda haki ili kupunguza migogoro pia aliwataka kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe kwa kutoa taarifa za uhalifu na kushiriki katika ulinzi wa maeneo yao kupitia vikundi vya ulinzi shirikishi.
Nao Viongozi wa eneo hilo wamelishukuru Jeshi la Polisi mkoa wa Songwe kwa maelekezo waliyopewa na wamehaidi kuyatekeleza kwa haraka ili kuondoa migogoro katika eneo hilo.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa