Na Heri Shaaban , TimesMajira Online
Wanawake katika Kata ya Gongolamboto wamezindua jukwaa lao la kiuchumi huku wakidhamiria kujengeana uwezo wa kijasiriamali na kufungua kiwanda.
Akizungumza wakati wa hafla ya kuzindua jukwaa hilo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake Kiuchumi Kata ya Gongolamboto, Neema Mchau, amesema lilizunduliwa rasmi mwaka 2019 na mwaka huu wanalihuwisha ili kuendeleza yale mazuri waliyokwisha yafanya .
Amesema tangu kuundwa kwa jukwaa hilo wamepata mafanikio mengi ikiwemo elimu ya ujasiriamali na kushiriki katika maonesho mbalimbali ya kitaifa pamoja na kupata mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri.
“Baada ya uhuwishwaji wa jukwaa hili tumedhamiria kuhamasisha wanawake waweze kujiunga kwenye vikundi na kuwatafutia wataalamu wa masuala ya teknolojia ili waweze kuvisajili.
Tuna lengo la kuweka wiki ya mafunzo ya ujasiriamali wanawake wapate ujuzi na zoezi hili litakuwa endelevu,” amesema Neema.
Amesema matarajio yao ni kupata kundi moja la kata ili waweze kufungua kiwanda cha jukwaa na kwamba hiyo ndiyo ndoto yao.
Hata hivyo amesema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile kukosa masoko kwa baadhi ya bidhaa wanazozalisha, riba kubwa kwenye taasisi za fedha na ucheleweshaji wa usajili na upatikanaji wa vyeti katika ngazi ya halmashauri.
Naye Ofisa Maendeleo wa Kata ya Gongolamboto, Hadija Omary, amewataka wanawake hao kuwa waaminifu wakati mikopo ya asilimia 10 itakapoanza kutolewa tena ili iweze kuwanufaisha wengi.
“Tukae kwa kutulia mambo yanarekebishwa, kuna vikundi vingi vimeomba mikopo lakini tunasubiri mwongozo kutoka ngazi za juu, kwahiyo endeleeni kuunda vikundi na kujishughulisha na shughuli mbalimbali za kiuchumi…lakini tukipewa fedha tuzirudishe,” amesema Hadija.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Gongolamboto ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo,Lucas Lutainurwa amewahakikishia wanawake hao kuwa ataendelea kushirikiana nao kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili ili wasonge mbele kiuchumi.
Amesema pia changamoto ya soko inafanyiwa kazi kwani Serikali ina mpango wa kujenga soko katika Mtaa wa Gulukwalala na kwamba usanifu umeshafanyika na michoro ipo tayari.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa