Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Lushoto
Baadhi ya wadau wa maji Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga wamesema dhamira ya Serikali ni kumtua mama ndoo kichwani, huenda isiweze kutimia kwenye Tarafa ya Mlalo kutokana na baadhi ya wananchi kuharibu mazingira kwa kulima kwenye moyo na vyanzo vya maji.
Wameyasema hayo kwenye mkutano wa Wadau wa Maji na Vyombo vya Watoa Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii (CBWSO’s) Tarafa ya Mlalo na Mlola Kata ya Ngwelo kwa uratibu wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Lushoto, kwa ajili ya kuunganisha vyombo hivyo ili viweze kuleta tija kwa jamii.
“Serikali inafanya jitihada za kumtua mwanamke ndoo kichwani, lakini kwa Tarafa ya Mlalo jambo hilo linaweza kushindikana kwa sababu ya uharibifu wa mazingira,kipaumbele cha kwanza cha maji ni kunywa binadamu siyo kunyweshea mashamba,”amesema Diwani wa Kata ya Mlalo Rashid Rajab maarufu Madagaa.
Meneja wa RUWASA Wilaya ya Lushoto Mhandisi Erwin Sizinga amesema wanaunganisha vyombo vya watoa huduma ya maji ili kuleta ufanisi na nguvu za kiutendaji.
Hivyo wameamua kuviunganisha vyombo kwa ngazi ya Tarafa na kutakuwa na vyombo vya watumia maji (CBWSO’s) saba kwenye Wilaya ya Lushoto kikiwemo cha Mlalo Wasso.
Mratibu wa CBWSO’s Mkoa wa Tanga Hans Mwiyola amesema viongozi wa vijiji na wadau wengine wa maji wana wajibu wa kuwahimiza wananchi kulipia maji ili kuwezesha Bodi za Maji ziweze kujiendesha na kuweza kufanyia ukarabati miradi ya maji huku akihimiza fedha zinazopatikana zipelekwe benki.
Katika mkutano huo ambao ulikwenda sambamba na uchaguzi wa viongozi wa Bodi ya Maji ya Mlalo Wasso, ambapo Waziri Ngereza alichaguliwa kuwa Mwenyekiti na kuahidi kupeleka maji kwenye vijiji vyenye shida ya maji ikiwemo Majulai kilichopo Kata ya Mwangoi.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa