November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi Korogwe watakiwa kulinda miundombinu ya umeme vijijini

Na Waandishi Wetu, Timesmajira Online

Naibu Waziri wa Nishati,Judith Kapinga ametoa wito kwa wananchi kulinda miundombinu ya umeme vijijini ili iendelee kuwa na thamani kwa sasa na vizazi vijavyo.

Kapinga ametoa wito huo Desemba 6,2023 Kata ya Makuyuni iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Vijijini mkoani Tanga wakati akikagua mradi wa kupeleka umeme awamu ya tatu, mzunguko wa pili, unaotekelezwa na Mkandarasi, kampuni ya Tontan Ltd chini ya usimamizi wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA).

“Mlinde miundombinu ya miradi hii ni ya thamani kubwa, tuoneshe ushirikiano kwenye utekelezaji wake kwani haina fidia na inagharamiwa kwa fedha nyingi, ikiwa na lengo la kupeleka huduma kwa wananchi hivyo niwaombe kutoa ushirikiano ili miradi isichelewe, kama eneo lako litatakiwa kupita nguzo toa ushirikiano kwa kuwa umeme unaopita hapo hauna madhara,”ameeleza Kapinga.

Aidha amebainisha kuwa, Serikali itaendelea kuleta fedha katika Jimbo hilo la Korogwe Vijijini na itazidi kusimamia miradi hiyo ikamilike kwa wakati ili wananchi wote wapate huduma ya umeme.

Pia amesema, Serikali itaendelea kuwasimamia kwa ukaribu wakandarasi wote waliopewa zabuni ya kutekeleza miradi ya kusambaza umeme vijijini ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa na kuwanufaisha wananchi kama ilivyopangwa.

Mbali na hayo Kapinga amewataka wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo kutenda haki kwa wananchi kwa kukamilisha miradi hiyo kwa wakati kwani kulegalega kwao kunakwamisha maendeleo kwa wananchi hao.

Kwa upande wake Msimamizi wa miradi ya REA Mkoa wa Tanga Mhandisi Balisidya Myula amebainisha kuwa Jimbo la Korogwe Vijijini lina jumla ya Kata 29, Vijiji 118 na Vitongoji 610 ambapo vijiji 91 sawa na asilimia 77 vilipatiwa huduma ya umeme kupitia Miradi ya REA III (Mzunguko wa Kwanza na wa Pili).

Hivyo vijiji 27 ambavyo havina umeme vinatarajiwa kuunganishwa na huduma ya umeme kabla ya Juni, 2024.

Akizungumzia Mradi wa REA III (Mzunguko wa Pili) katika Kijiji cha Sharaka, Mhandisi.Myula amesema mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya milioni 151.5 na Mkandarasi (Kampuni ya Tontan Ltd) umekamilika kwa asilimia 80 na kazi iliyobaki inatarajiwa kumalizika ifikapo Tarehe 31 Desemba, 2023.

Mhandisi Myula ameitaja miradi mingine inayotekelezwa katika Jimbo la Korogwe vijijini ni pamoja na mradi wa kupeleka umeme kwenye Migodi midogo na maeneo ya Kilimo,mradi wa kupeleka umeme kwenye bituo vya afya na pampu za maji na mradi wa PERI Urban III.

Nae Msimamizi wa miradi kutoka kampuni ya Tontan Ltd, Mhandisi, Lomayan Mollel amewaomba radhi wananchi kwa kuchelewesha utekelezaji wa mradi huo na kuahidi kuwa utakamilika ifikapo Desemba 31, 2023.