Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
MRADI wa Vijana Kilimo Biashara (VKB) unaotekelezwa na Shirika la Small Enterprises Institutional Development (SEIDA) kwa kushirikiana na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) unatarajia kunufaisha vijana zaidi ya 20, 000 wa Mikoa ya Tabora na Shinyanga ili kuwainua kiuchumi.
Mradi huo umetambulishwa na Meneja wa Mradi Frank Godlight Lyimo katika warsha ya siku moja iliyofanyika jana katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora
na kuhudhuriwa na Maafisa Maendeleo ya Jamii na Maafisa Kilimo kutoka wilaya za Igunga, Uyui, Nzega na Sikonge.
Godlight amesema mradi huo wa kimkakati unatarajiwa kutekelezwa katika jumla ya halmashauri 8 za Mikoa hiyo miwili.
Ametaja halmashauri hizo kuwa ni Igunga, Nzega, Uyui, Sikonge na Tabora Manispaa za Mkoani Tabora na Kishapu, Msalala, Ushetu na Shinyanga Vijijini za Mkoani Shinyanga.
Amebainisha kundi litakalonufaika na mradi huo kuwa ni vijana wa kike na kiume walio na umri kati ya miaka 18-35, asilimia 70 ya wanufaika hao ni wanawake na asilimia 70 vijana.
Godlight amefafanua kuwa kwa Mkoa wa Tabora jumla ya vijana 15,000 watahusika katika mradi huo na 10, 000 kwa Mkoa wa Shinyanga.
‘Mradi huu ni wa miaka 3 na utekelezaji wake umeanza Oktoba 2023 hadi Septemba 2026 na mazao makuu yatakayolimwa ni alizeti, mtama na Mbogamboga,’ ameeleza.
Meneja amesisitiza kuwa wanufaika watawezeshwa kuongeza kipato na kufanya uzalishaji wenye kukidhi mahitaji ya soko, kuhamasisha matumizi ya mbegu bora, kupunguza upotevu wa mazao wakati na baada ya mavuno na kufikia makundi ya watu wenye mahitaji maalumu pia.
‘Lengo kuu la mradi huu ni kuongeza kipato cha wakulima wadogo hususani vijana wa kiume na wa kike,’ ameongeza.
Aidha kipato cha kaya na jamii kitaongezeka kupitia wingi wa mazao yatakayozalishwa na nafasi za ajira pia zitapatikana kupitia mnyororo wa thamani wa mazao ya alizeti na mtama.
Meneja ameishukuru serikali kupitia Wizara ya TAMISEMI na Ofisi za Makatibu Tawala wa Mikoa hiyo 2 kwa ushirikiano mkubwa waliowapa tangu kwenye maandalizi hadi sasa.
Awali akifungua warsha hiyo Afisa Kilimo wa Mkoa huo Modest Kaijage amelipongeza Shirika la SEIDA na WFP kwa kuleta mradi huo Mkoani humo kwa kuwa mazao hayo yanalimwa katika maeneo mengi.
Amewataka vijana wa kiume na kike kuchangamkia mradi huo na ajira zitakazotolewa ili kujikwamua kiuchumi.
Amebainisha kuwa kupitia mradi huo uzalishaji wa mtama na mafuta ya alizeti utaongezeka sana katika mkoa huo hivyo kuinua uchumi wa wananchi.
More Stories
Rais Samia kuzindua mfuko wa kuendeleza kazi za wabunifu
Makalla ampongeza Lissu kukiri CHADEMA haina wagombea Serikali za Mitaa
Chande azindua misheni ya uangalizi uchaguzi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika