November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi wahamasishwa kujitokeza kuchangia damu Tumbi

Na Mwandishi wetu,Pwani

MKUU wa Kitengo cha Damu Salama kutoka Hospitali ya Mkoa Pwani Tumbi,Tatu Gemela ametoa wito kwa wananchi mbalimbali nchini kuungana na wananchi wa Mkoa wa Pwani siku ya Disemba 9,2023 katika kuchangia damu ili kuweza kuokoa maisha ya majeruhi

Akizungumza jana mkoani Pwani,Mkuu huyo wa kitengo, Gemela amesema hospital hiyo imekuwa na kawaida ya kupokea watu mbalimbali katika kuchangia Damu kwani ni hospital ambayo ipo katikati ya barabara kubwa.

Amesema mahitaji kwa siku wanatumia chupa 15 ambayo kwa mwezi ni sawa na chupa 450 wamekuwa wanaotumia chupa nyingi hivyo ni muhimu watu sasa kuwa Wazalendo katika kuchangia Damu na kuokoa maisha ya wengine.

“Kuelekea Disemba 9 siku ya uhuru nchini,tunawakaribisha wananchi wote wa Mkoa wa Pwani kuja kuchangia damu ili kuokoa maisha ya watu wengine tunawakaribisha watu mbalimbali kuanzia miaka 18 hadi 60 kuja kuwatolea wenzetu damu,”amesema na kuongeza

“Watu waje kuonyesha uzalendo wao kwa kuchangia damu maana tunatumia Damu nyingi na hii itasaidia kuokoa maisha ya mama anaejifungua ,watoto wadogo hasa wale walio chini ya miaka mitano pamoja na majeruhi wa ajali ukizingatia hospitali yetu ndo ipo katikati,”amesema.