October 9, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Prof. Mkenda: Masomo ya dini ni ya kipekee

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online no

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amezindua Tanzania Islamic Studies Teaching Association (TISTA) huku akisisitiza kuwa katika hatua za uandaaji wa mitaala waliona upo umuhimu wa kuwashirikisha katika eneo la imani ili kwa pamoja wasaidiane kuja na mitaala itayokuwa na manufaa kwa wananchi bila kuharibu imani za watu.

Prof. Mkenda amesema hayo Novemba 30, 2023 katika uzinduzi huo ulioenda sambamba na makabidhiano ya muhtasari na kitabu cha kwanza cha Mwanafunzi cha Elimu ya dini ya Kiislamu, tukio lililofanyika katika ukumbi wa Mfalme Mohamed BAKWATA makao makuu Kinondoni Dar es Salaam.

Ambapo amebainisha kuwa, elimu inayotolewa kupitia masomo ya dini ni tofauti na ile ya masomo mengine kwani elimu hiyo inahusisha masuala ya imani na hugusa zaidi hisia.

“Mitaala ya dini ni ya kipekee, ni tofauti na mitaala ya somo la kemia ambayo unaweza kuchukua Wataalamu wa somo hilo ukaangalia na wa nchi nyingine ukaitengeneza, tofauti na ya dini inayovuta hisia na ikatokea tafsiri ambayo si sahihi inaweza kuibuka hisia kali sana”. Amesema Prof. Mkenda.

Aidha, Prof. Mkenda amemshukuru Mufti wa Tanzania Shekh Abubakar Zuberi na Mufti wa Zanzibar na timu zao kwa ushirikiano wanaoendelea kuuonesha katika kufanikisha adhima ya mtaala huo wenye manufaa kwa taifa.

Sambamba na hilo, Prof. Mkenda amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kusisitiza uboreshaji wa mitaala mipya utaomsaidia mwanafunzi kujiajiri au kuajiriwa pindi tu atapomaliza elimu.

Nae, Mufti Mkuu wa Tanzania Shekh Abubakar Zuberi amesema, uandaaji wa mtaala huo umeshirikisha umma wa waislamu wote kutoka Tanzania na Zanzibar hivyo kuufanya muhtasari huo kubeba taswira ya michango, mawazo ya waislamu wote nchini.

Ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Taasisi ya Elimu Tanzania kwa uongozi sahihi ya uliofanyika wa kuweka masomo ya dini katika mtaala huo mpya.