Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online
HOSPITALI ya Taifa Muhimbili imepokea msaada Milioni 15 kutoka Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) kwa lengo la kuwasaidia watoto wanaogua Saratani wanaopatiwa matibabu hispitalini hapo.
Akipokea msaada huo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali ya Muhimbili Dkt. Julieth Magandi amesema matibabu ya saratani yanagharama kubwa hivyo jamii haina budi kuchangia huduma na kwa wale wenye uwezo kujitokeza kuwasaidia wenye uhitaji ili huduma hizi ziwe endelevu.
Amesema Hospitali inawahudumia watoto wenye saratani ambao wengine wanaishi ndani ya hospitali kutokana na matibabu yao kuchukua muda mrefu.
‘‘Ninatoa wito kuwasaidia wenye uhitaji kwani matibabu ya kibingwa yanagharama kubwa”, amesema Dkt. Magandi.
Natumia fursa hii kutoa wito kwa jamii kujiunga na bima ya afya ili kuweza kumudu gharama za matibabu ’’ameeleza Dkt. Magandi
Awali akizungumza kabla ya kukabidhi hundi , Mkurugenzi Mkuu wa NBAA, CPA Pius Maneno amesema kila mwaka wana utaratibu wa kurejesha kwa jamii kwa mwaka huu wameona ni vema wakawagusa watoto wanaoumwa saratani ambao wamelazwa Muhimbili.
‘’Nimesimama hapa kuwawakilisha wahasibu na wakaguzi wa Tanzania, tunaahidi kuendelea kushirikiana na MNH katika kuboresha utoaji wa huduma za afya, pia tunapongeza mabadiliko makubwa yaliyofanyika Muhimbili najua hii ni juhudi ya Serikali ya kuboresha huduma za afya pia haya yote yamefanikiwa kutokana na uongozi mzuri wa Muhimbili’’amesema CPA Maneno
Naye Mkurugenzi wa Fedha na Mipango Muhimbili CPA Ashraph Abdulkarim ameishukuru NBAA kwa msaada huo na kuomba bodi zingine kuguswa na kujitokeza kuchangia huduma za afya.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi