Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko ametunuku vyeti ngazi mbalimbali kwa wahitimu 439 wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka, mkoani Kilimanjaro.
Dkt. Biteko, amewaasa kuwa chochote watakachofanya kuchukia rushwa, kutojitajirisha katikati ya hali ngumu za wananchi na walinde maliasili za nchi kwa wivu mkubwa na kuwa Walinzi wa wenzao.
Amesema hayo Novemba 25 mwaka huu, wakati alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan katika Mahafali ya 59 ya Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka, mkoani Kilimanjaro ambapo Mahafali hayo yameenda sambamba na Kilele cha Maadhimisho ya Miaka 60 ya Chuo hicho.
“Chuo hiki ni kiungo muhimu katika Sekta ya Maliasili na Utalii, kuanzishwa kwake kulitokana na tamko la Baba wa Taifa, Hayati, Mwl. Julius Kambarage Nyerere katika Kongamano la Uhifadhi wa Wanyama Pori mwaka 1961.
Kupitia tamko hilo alionesha dhamira na utayari wake wa kuifanya Afrika kuwalinda wanyama na mazingira yao kwa kizazi kilichopo na vizazi vijavyo, hivyo nyinyi ndio mnaoendeleza kazi lengo hilo la Baba wa Taifa,” amesema Dkt. Biteko.
Amesema, Chuo hicho pia ni kielelezo cha ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na nchi nyingine duniani kwani Chuo hicho kinapata wanafunzi kutoka nchini mbalimbali duniani.
Aidha, amesema Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan anatambua mchango wa Chuo hicho katika ukuaji wa Sekta ya Maliasili na Utalii nchini na hivyo ameahidi kuwa kama kuna changamoto zozote Serikali itazichukua na kuzifanyia kazi.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kusimamia vyema sekta ya Maliasili na Utalii.
Amesema, ni kiungo kikubwa kwenye uchumi wa nchi kwani bila Sekta hiyo mapato na fedha zinazohitajika kuendeleza miradi mbalimbali zinaweza kuwa na changamoto ya upatikanaji.
Hata hivyo amesema, Utalii unachangia takriban asilimia 21 ya Pato la Taifa, na asilimia 25 ya fedha za kigeni, pia ni chanzo kikubwa cha ajira nchini kwani unachangia ajira milioni 1.5 na zaidi ya asilimia 11 ya ajira zote hapa nchini.
Dkt. Biteko ameongeza kuwa, asilimia 80 ya Utalii nchini unatokana na Wanyama pori, ambao wametokana na mazingira yetu tuliyoyahifadhi, mapori ya akiba, mapori tengefu, misitu pamoja na hifadhi za wanyama.
Katika Mahafali hayo wahitimu 439 walitunukiwa vyeti katika ngazi mbalimbali za masomo ikiwemo Shahada ya Uzamili ya Mipango na Usimamizi wa Utalii, Shahada ya Usimamizi wa Wanyamapori, Stashahada ya Juu ya Utalii wa Wanyamapori, Astashahada ya Usimamizi wa Wanyamapori na Cheti cha Msingi cha Usimamizi wa Wanyamapori.
Mahafali hayo yalihudhuriwa na Viongozi mbalimbali akiwemo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu na Balozi wa Msumbiji nchini Tanzania, Ricardo Mtumbuida.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi