Na Moses Ng’wat,Timesmajiraonline,Ileje
MKUU wa Wilaya ya lleje Farida Mgomi kwa kushirikiana na wazazi wamefanikiwa kumrejesha shuleni, Irene Mwazembe, mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule ya sekondari ya wasichana (Ileje Girls) aliyekatisha masomo na kwenda kufanya kazi za ndani katika Mji wa Tunduma baada ya wazazi wake kudaiwa kushindwa kumudu kuchangia gharama za chakula shuleni hapo.
Hatua ya Irene kurejeshwa shule hapo imekuja ikiwa ni siku chache baada ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dkt Francis Michael kumuagiza Mkuu wa Wilaya hiyo, kuhakikisha anamrejeaha shuleni mwanafunzi huyo wa kidato cha kwanza ili aendelee na masomo.
Mbali na Irene, pia Mkuu wa Mkoa Dkt. Francis ameagiza kurejeshwa shuleni hapo kwa wanafunzi wengine watatu ambao wazazi wao waliwahamisha na kuwapeleka katika shule za kutwa kwa kisingizio cha wazazi kukosa michango ya chakula.
Akimkabidhi mwafunzi huyo kwa uongozi wa shule mbele ya Mkuu wa Mkoa, jana Novemba 20, 2023, Mkuu wa Wilaya ya Ileje Mgomi alisema jitihada za kumrejesha shule mwanafunzi huyo zimetokana na wazazi kukubali na kutoa ushirikiano kwake.
“Mkuu wa Mkoa kurejea kwa mwanafunzi huyu ni faraja Kwa uongozi wa Wilaya kwani ni adhima ya serikali kuhakikisha kila mtoto wa kitanzania anapata haki ya msingi ya kusoma kwani lengo la kuanzishwa Kwa shule ya wasichana wilaya ya Ileje ilikuwa ni kuwakomboa watoto wakike” alisema Dc Mgomi.
Kuhusu wanafunzi wengine waliondolewa shuleni hapo DC Magomi amesema jitihada za wanafunzi wawili kurejeshwa shuleni hapo zinaendelea, huku mwanafunzi wa tatu yeye alihamishiwa mkoani Morogoro ambako anaendelea vizuri na masomo baada ya kuchukuliwa na baba yake mdogo.
Hata hivyo, baada ya Mkuu wa Mkoa kushuhudia kurejeshwa kwa mwanafunzi huyo na kukabidhiwa kwa walimu.
Mkuu huyo wa Mkoa Dkt. Francis alilazimika kutoa maelekezo mahususi kwa ofisa elimu wa Mkoa huo Michali Lugola kuhusu wanafunzi wa kike katika mkoa wa Songwe, akimtaka kuhakikisha anafanya zoezi la kutembelea shule zote za bweni za wasichana ili kubaini wanafunzi walioacha shule kwa kukosa fedha za chakula ili wawarejeshe kama ilivyofanyika katika shule ya wasichana Ileje.
Kwa mujibu wa Kaimu Mkuu wa shule hiyo, Sharon Kadinde, shule ya wasichana iliyoanzishwa mwaka huu ilipangiwa wanafunzi 75 , lakini walioripoti shuleni hapo ni 71 tuu.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa