Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeshauri wakulima na wafugaji kuimarisha miundombinu ya shughuli zao na kudhibiti visumbufu vya mimea na mifugo ili kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za el-nino.
Aidha wameshauriwa kutumia mbinu bora za kilimo na teknolojia ya kuzuia maji kutuama mashambani, kuzuia mmomonyoko wa udongo na upotevu wa rutuba huku wafugaji wakitakiwa kutunza vizuri malisho yao.
Ushauri huo umetolewa hivi karibuni na Meneja wa Mamlaka hiyo Kanda ya Magharibi Waziri Omari alipokuwa akiongea na viongozi mbalimbali wakiwemo wadau wa maendeleo Mkoani Tabora.
Alisema Mamlaka hiyo kupitia Mkurugenzi wake Mkuu imeshatoa utabiri wa kuwepo mvua za juu ya wastani hadi wastani zinazotarajiwa kuanza kunyesha wiki ya kwanza ya mwezi Novemba 2023 hadi mwishoni mwa Aprili 2024.
Alibainisha kuwa kati ya mwezi Novemba 2023 na Januari 2024 kunatarajiwa kuwa na mvua nyingi zilizo juu ya wastani na mifumo ya TMA inaonesha uwepo wa mvua za el-nino ambazo zinaweza kuleta athari kubwa.
Omari alifafanua kuwa el-nino ni hali ya ongezeko la joto juu ya wastani, ila haimaanishi kwamba joto hilo litasababisha mvua nyingi, mvua nyingi huchangiwa na mifumo mingi ya hali ya hewa ikiwemo ongezeko la joto baharini.
Alisema katika kipindi hicho shughuli za kiuchumi zitaendelea kama kawaida ikiwemo kilimo na ufugaji ila kina cha maji cha mito na mabwawa kitaongezeka na magonjwa ya mlipuko yanaweza kujitokeza kutokana na uchafuzi wa maji.
‘Natoa wito kwa wakulima, wafugaji na wadau wengine kuchukua tahadhari wanapoendelea kutekeleza shughuli zao kutokana na athari zinazoweza kujitokeza katika kipindi hicho’, alisema.
Akiongea kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo Balozi Dkt Batilda Burian, Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mjini Luis Bura aliwashukuru TMA kwa kuwapa semina hiyo kwani itasaidia wakulima, wafugaji na sekta nyingine kuchukua tahadhari.
Alielekeza Wakurugenzi wa Halmashauri zote Mkoani humo kuhamasisha Mamlaka ya Mbolea (TFRA) na Mawakala wa Usambazaji Mbolea kusogeza huduma hiyo karibu zaidi na wananchi.
Aidha alishauri vyama vya ushirika kujisajiri kuwa mawakala wa kuuza mbolea na kuwataka wakulima kuanza kuandaa mashamba yao mapema na kutumia mbegu bora zinazostamili mabadiliko ya tabia ya nchi.
More Stories
Bei za mafuta Novemba 2024,zaendelea Kushuka
TARURA yaomba Mkandarasi aitwe
Ilemela yakusanya bilioni 3.7.robo ya kwanza