Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
-Zawadi za pesa taslimu na pikipiki kutolewa kila wiki
Benki ya NMB Kanda ya Kusini imezindua kampeni maalum kwa wakulima wa kanda hii ijulikanayo kama Bonge la Mpango mchongo wa kilimo.
Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Kusini, Faraja Ng’ingo alisema kuwa benki hiyo imekuja na kampeni hiyo ili kuendelea kuhamasisha matumizi ya huduma za benki kwa wakulima na vyama vya msingi.
Alisema NMB inatambua na kuuthamini mchango mkubwa wa biashara ya kilimo kwa kanda ya kusini hususani kilimo cha korosho katika ustawi wa benki hiyo na kanda ya kusini hususan mikoa ya lindi na Mtwara.
Akizungumzia kampeni hiyo alisema mkulima wa korosho sasa akipokea fedha za mauzo kupitia Benki ya NMB mbali ya huduma bora anaweza kuwa miongoni mwa washindi mbalimbali wa zawadi ambazo benki ya NMB imetenga kwa ajili ya kampeni hii.
NMB imetenga pikipiki tano kwa ajili ya wakulima ambapo kila mwisho wa wiki kutaendeshwa droo ya kutafuta mshindi atakaejinyakulia pikipiki hiyo. Droo hii itaendeshwa kwa kipindi cha wiki tano. Pia wakulima wengine watano watajinyakulia fedha taslimu kiasi cha shilingi 100,000 kila mmoja katika kila droo.
“Maana yake ni kwamba kila wiki tutashuhudia wakulima watano wakijishindia pesa taslimu itakayowekwa katika akaunti zao pamoja na mmoja kujishindia pikipiki” alisema Meneja wa Kanda ya Kusini.
Ili mtu ashinde zawadi hizo anatakiwa kuwa na akaunti ya Benki ya NMB, ajishughuliishe na biashara katika mnyororo wa thamani ya Kilimo na apitishe mauzo yake katika Benki ya NMB.
Akizungumza katika tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abass Ahmed aliipongeza Benki ya NMB kwa kuendeleza kampeni hii ya kuhamasisha wakulima kutumia Benki katika kupokea malipo ya mauzo ya mazao yao.
Alisema wakulima wengi wamekuwa wakikutana na maswahibu mbalimbali katika kipindi hiki hasa yanayo husiana na uhalifu sababu ya kukaa na fedha nyingi ndani mwao badala ya kuzihifadhi sehemu salama kama Benki ya NMB.
“Fedha hizi zinazowekwa kwenye akaunti ni za kwetu, kwa usalama wa fedha zetu na hata akiba ni kwa ajili yetu, lakini wao wanakupa zawadi, hili ni jambo kubwa sana. Kwa walio na Akaunti za NMB changamkieni fursa na wasio na akaunti, muda ndio huu kafungueni akaunti haraka sana muanze kuzitumia na mjishindie mazawadi kemkem kutoka benki ya NMB” Kanai Ahmed Abbas.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa