November 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Asilimia 95 ya vijiji Buhigwe vyapata huduma ya maji safi

Na Allan Vicent, TimesMajira Online

SERIKALI ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imefanikiwa kufikisha huduma ya maji safi na salama ya bomba katika jumla ya vijiji 41 kati ya 44 vilivyopo katika Wilaya ya Buhigwe Mkoani Kigoma.

Hayo yamebainishwa jana Kaimu Meneja wa Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira (RUWASA) wilayani humo Francis Molel alipokuwa akiongea na vyombo vya habari ofisini kwake.

Amesema mafanikio hayo yametokana na juhudi kubwa zinazofanywa na serikali ya Rais Samia na dhamira yake ya dhati ya kuwatua akinamama ndoo kichwani.

Amefafanua kuwa dhamira hiyo imewezesha kata zote kuwa na miradi ya maji inayotoa huduma kwa wananchi na hata vijiji 3 vilivyobakia vya Nyaruboza, Rusaba na Nyamiyaga tayari vimetengewa bajeti kwa mwaka huu wa fedha.

Molel amebainisha baadhi ya miradi ya kimkakati iliyokamilika hivi karibuni kuwa ni wa vijiji 4 vya Kavomo, Buhigwe, Mlera na Mji wa Kiserikali wa Bwega.

Amebainisha kuwa mradi huo uliogharimu sh bil 1.6 umekamilika kwa asilimia 100 na kuanza kutoa huduma kwa wakazi zaidi ya 20,000.

Mradi mwingine ni wa Kijiji cha Migongo katika kata ya Kilelema ambao umegharimu sh mil 963 na umeanza kutoa huduma kwa wakazi zaidi ya 15,000 wa Migongo na unatarajiwa pia kuhudumia wakazi wa Kijiji cha Kilelema.

Ametaja mradi mwingine wa kimkakati unaoendelea kutekelezwa kuwa ni wa kata 4 za Kibande, Mkatanga, Mnanila na Kibwigwa wenye thamani ya sh 8.2.

Molel amebainisha kuwa mradi huo unaotarajiwa kukamilika mwezi Februari mwakani utanufaisha wakazi wa vijiji 8 vilivyoko katika kata hizo.

Ametaja vijiji hivyo kuwa ni Usagara, Kitambuka, Mkatanga, Nyakimwe, Kibwigwa, Bweranka, Mnanila na Kibande.

Wakazi wa Wilaya hiyo Shakari Yahaya wa Kijiji cha Nyankoronko na Muyabho Lulamye wa Kijiji cha Kavomo wamemshukuru Rais Samia kwa kujali wananchi wake na kupeleka fedha nyingi vijijini ili kuharakisha maendeleo ya jamii.