Na Penina Malundo, timesmajira
MTENDAJI Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Mohamed Besta amefungua mafunzo ya Wahandisi wapya walioajiriwa na Serikali kupitia TANROADS wapatao 49 ambao watapelekwa kufanya kazi sehemu mbalimbali Nchini ili kupunguza uhaba wa watumishi wa kada hiyo katika sekta ya Ujenzi.
Akizungumza muda mfupi baada ya kufungua mafunzo hayo yaliyoanza Oktoba 30,2023 katika Ukumbi wa Kobe Sabasaba Jijini Dar- es Salaam Mhandisi Besta amesema ni muendelezo wa hatua mbalimbali ambazo zinachukuliwa na Serikali kuwawezesha na kuwaongezea uwezo wa kitaaluma Wahandisi ili waweze kusimamia vizuri kazi za ujenzi wa miundombinu ya barabara na Madaraja.
Amesema mafunzo haya yamefanyika kuwaongezea chachu na kupata Wahandisi wapya wenye ueledi lengo ni kuimarisha utendaji kazi hasa katika usimamizi wa viwango katika ujenzi wa barabara.
“Nachukua fursa hii kumshukuru Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, Wizara ya Ujenzi na Serikali kwa ujumla kwa kutoa kibali kwa TANROADS kuajiri Wahandisi wapya kabisa ambao wataenda kuongeza ufanisi hasa katika maeneo ambayo Wahandisi wametoka kwa kustaafu ama kuhamia maeneo mengine”, amesema na kuongeza
“Lazima tuwajenge Wahandishi wapya ninawataka wafahamu kwamba wanaenda kuhudumia miundombinu ya takribani Kilomita 36,760 nchi nzima pamoja na miradi mingi inayoongezeka sio katika ngazi ya Kitaifa tu lakini vilevile katika ngazi ya Mikoa kwa hiyo baada ya mafunzo haya nina amini watakuwa wamejiweza, tutaendelea kuwasimamia na kutoa mafunzo ya namna hii mara kwa mara ili kuendelea kuwajengea uwezo kwa jinsi ambavyo teknolojia inavyoendelea kubadilika’’amesema.
Kwa Upande wake Meneja Rasilimali watu na Utawala wa TANROADS,Pilika Kasanda alisema watumishi hao wapya ambao wameajiriwa kuanzia Oktoba Mwaka huu ni muendelezo wa utekelezaji wa maelekezo ya Rais Dkt. Samia ambaye ameridhia TANROADS kuajiri jumla ya watumishi 125 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hususani miradi mipya ambayo inaendelea kutekelezwa na Serikali ikiwemo ile ya EPC + F.
Amesema Rais Dkt. Samia ametoa kibali kuajiriwe kwa Wahandisi 63 na Mafundi 62 katika kibali hicho awamu ya kwanza wamepata Wahandisi 49 ambao wameanza kufanyiwa taratibu za awali za ajira.
“Tulianza na mafunzo ya utayari wa kuajiriwa kwenye utumishi wa Umma na leo tumeendelea na mafunzo ya Kitaaluma ambayo yametolewa na wakufunzi wetu wa ndani lengo ni kuwawezesha na kuwajengea uwezo Wahandisi hawa wapya kabla ya kwenda kufanya kazi kwenye maeneo mbalimbali ya Mikoa ya Tanzania bara,”amesema.
Kwa upande wake Mkuu wa kitengo cha Utafiti na Maendeleo kutoka Maabara Kuu ya Utafiti Wakala wa Barabara Tanzania Mhandisi Mussa Omari Mataka amesema mafunzo hayo yameanza Oktoba 30 na yanatarajiwa kumalizika Novemba 11 mwaka huu 2023.
Amesema mafunzo hayo yatajumuisha maeneo yote makuu ya ujenzi wa barabara “Ujenzi wa barabara unaongozwa na miongozo kadhaa ambayo ndio inayoelekeza taratibu zote za ujenzi kwa hiyo katika mafunzo haya tutawapitisha kwenye miongozo hiyo lakini zaidi tutapita katika mwongozo mkuu ambao ni Usanifu ambao unatoa maelekezo yote ili kupata Barabara bora’’.
“Tunatarajia hawa Wahandisi wakishamaliza mafunzo haya wawe wameshaelewa yale mambo muhimu ya awali yanayohusu usimamizi wa viwango vya ujenzi, vifaa na malighafi za ujenzi ambapo tunategemea Mhandisi atakuwa na uwezo wa kuona zile shida ndogo ambazo zinajitokeza kwenye maeneo ya miradi; huu sio mwisho tutarajia huko mbele waje ili wapate mafunzo kwa kina zaidi kwa sababu eneo la ujenzi wa barabara ni pana’’ amesema Mhandisi Mussa.
More Stories
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â