November 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TASAC yawataka wadau kuzingatia sheria, wanapoingiza bidhaa zao

Na Agnes Alcardo, Timesmajira, Online Dar es Salaam

SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limewataka wadau mbalimbali wanaohusika na uingizaji wa mafuta ya kemikali kwenye Bandari ya Dar es Salaam, kuhakikisha wanafuata taratibu, kanuni na sharia zilizopo ili waweze kufanya kazi zao bila kupata vikwazo vyovyote.

Wito huo umetolewa mwishoni mwa wiki na Kaimu Meneja Ugomboaji wa Shehena kutoka Shirika la uwakala wa Meli Nchini (TASAC), Michael Polycarp alipokuwa akitoa ufafanuzi juu ya utendaji wa kazi unaofanywa ndani ya Shirika hilo.

Amesema, wadau hao wakizingatia bidhaa tano zinazotolewa na TASAC wataweza kufanya kazi zao kwa weledi na kuinua mapato yao yanayotokana na kazi wanazozifanya kwa kufuata sheria zilizopo.

“Tunawaomba wadau wetu kuzingatia bidhaa zetu tano na kufuata sheria, kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia kufanya kazi zao bila ya kuwepo kwa vikwazo vyovyote na kulisaidia shirika kuendelea kufanya vizuri katika utendaji kazi wake,” amesema Polycap.

Akizungumzia kuhusiana na changamoto wanazozipata kwa wateja wao pamoja na taasisi zinginezo wanazofanya nazo kazi, Kaimu Meneja wa TASAC amesema ni pamoja na kuwemo kwa baadhi ya mifumo ya utoaji wa mizigo hiyo kutosomana kwa wakati.

Nao baadhi ya wadau waliyohudhuria katika mkutano huo akiwemo, Neema Molel kutoka kampuni ya Seafooth General Agencies L.t.d, amelipongeza Shirika hilo kwa kuwatatulia changamoto zao kwa wakati.

Kwa upande wake, John Akuti ambaye ni mwakilishi kutoka kapuni Oxley L.t.d, amesema, mbali na Shirika hilo kuwafnaya vizuri lakini bado wamekuwa wakikabiliwa na changamoto nyingine hususani wanapokuwepo bandarini.