November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mfumo wa ukataji tiketi kidigitali wazinduliwa

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Kampuni ya Hashtech Technologies Limited imezindua mfumo wa ukataji tiketi kidigitali kupitia Aplikesheni ya MySafari ambayo inampa abiria nafasi ya kupata bima ya maisha ya Jubilee bure kipindi chote atakapokuwa safariini.

Kampuni ya bima za Maisha ya Jubilee imetumia fursa hiyo ya uzinduzi kutoa elimu ya bima za maisha kwa abiria na umuhimu wake kwani inampa abiria amani ya moyo kwa kujua kwamba analindwa maisha yake wakati wote wa safari.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mtendaji Mkuu Jubilee Insurance, Hellena Mzena amesema ” Uzinduzi huu Si kuhusu programu ya Kiganjani ya My safari tu, lakini pia unarahisisha ukataji tiketi ikiwa ni pamoja na kumpa msafiri ulinzi wa maisha yake pindi akiwa safarini bila malipo kwa kila abiria anaenunua tiketi kupitia programu hii , hivyo Kila anaekata tiketi kupitia My safari anakua amepata bima ya maisha “

Naye Mkurugenzi Mtendaji HASHTECH Zena Msonde amesema “hatujarahisisha tu ununuzi wa tiketi za mabasi bali pia tumehusisha suala muhimu la usalama wa watumiaji wa mtandao wa My safari wanapokuwa safarini”

“Tunafuraha kutambulisha kipengele ambacho hakijawahi kuonekana katika ulimwengu wa usafiri nchini Tanzania, uwezekano wa Bima ya Maisha bila malipo ya ziada kwa kila abiria anayetumia app hiyo”

Mkurugenzi kutoka LATRA CCC, Leon Ngowi amesema Aplikesheni hiyo itasaidia sana kuondoa changamoto zilizopo kwenye usafiri kwani kwenye vituo vingi vya mabasi kumekuwa na udalali mwingi.

“Kupitia App hii tutaondoa mfumo usio rasmi wa ajira na watu wataanza kuwa mawakala wanaoeleweka kupitia huduma hii mpya”

Katibu Mkuu kutoka TABOA, Priscus Joseph mepongeza kwa kuletwa Aplikesheni hiyo kwani ni ya msaada mkubwa kwa abiria na dereva kwani itasaidia kupunguza upotevu wa muda wa kwenda kituoni kukata tiketi lakini pia kuepuka kutapeliwa na watu wa barabarani.

Jubilee Life ni kampuni kinara ya bima hapa nchini kwa utoaji wa bima za maisha ambazo zimekua msaada mkubwa kwa Watanzania kwani zinahakikisha utimiaji wa ndoto zao hata kipindi ambacho hawatakuwepo.