Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya
JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Kikosi kazi cha Tume ya madini, linawashikilia watu watano kwa tuhuma za kutorosha madini na kufanya biashara ya madini bila kuwa na kibali.
Watuhumiwa waliokamatwa ni Masunga Kidishi [43], Timoth Simbu [26], Ngunje Ideshi [41], Ester John [25] na Baraka Silwani [28] wote wafanyabiashara na wakazi wa Chokaa Wilaya ya Chunya.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 28, 2023, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishina Msaidizi wa Polisi Benjamin Kuzaga amesema watuhumiwa walikamatwa Oktoba 26, 2023 huko Mtaa wa Kibaoni Wilayani Chunya wakiwa na madini aina ya dhahabu vipande 160 vyenye uzito wa gramu 6,933.6 wakiwa hawana nyaraka “Transport permit” wakiwa wanatorosha madini hayo kwenda kuuza nje ya mfumo wa Soko la dhahabu.
Aidha, dhahabu vipande 145 vilipatikana baada ya kupekua kwenye makazi ya mtuhumiwa Ngunje Ideshi. Awali kabla ya kukamwatwa vipande hivyo vilikamatwa vipande 15 vya dhahabu kwenye gari T.796 DTT IST iliyokuwa na watuhumiwa Timoth Simbu na Ngunje Kidishi. Watuhumiwa wanaendelea kuhojiwa na mara baada ya upelelezi kukamilika watafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.
Sambamba na hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia wahamiaji haramu 11 raia wa Ethiopia wote wanaume kwa kosa la kuingia nchini bila kuwa na kibali.
Watuhumiwa walikamatwa Oktoba 27, 2023 huko eneo la Igawa Wilaya ya Mbarali katika barabara Kuu ya Mbeya – Njombe wakati Askari wakiwa doria.
Watuhumiwa walikuwa wakisafirishwa kwa kutumia gari T.732 CRB Toyota Mark X rangi nyeupe ambalo lilikuwa likiendeshwa na Dereva Frank Makunde [38] Mkazi wa Makambako Mkoa wa Njombe ambaye pia amekamatwa kwa hatua zaidi za kisheria. Ufuatiliaji zaidi unaendelea ili kuwabaini wasafirishaji wengine pamoja na mmiliki wa gari hiyo.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa wafanyabiashara ya madini kufuata utaratibu wa kuuza na kununua madini katika masoko yaliyopo kwa mujibu wa sheria ili kuepuka usumbufu.
Kuzaga amesema Jeshi la polisi linatoa rai kwa wananchi kuacha mara moja kujihusisha na biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu [Wahamiaji haramu] kwani ni kinyume cha sheria, watakamatwa na kufungwa gerezani hivyo ni vyema wakatafuta kazi nyingine za kufanya ili kujipatia kipato halali.
More Stories
Rais Samia kuzindua mfuko wa kuendeleza kazi za wabunifu
Makalla ampongeza Lissu kukiri CHADEMA haina wagombea Serikali za Mitaa
Chande azindua misheni ya uangalizi uchaguzi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika