Na Allan Vicent, TimesMajira Online
RAIS wa awamu ya 6 Dkt Samia Suluhu Hassan ameipatia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kibondo (KIUWASA) kiasi cha sh bil 1.49 ili kutekeleza mradi wa ujenzi wa tanki kubwa litakalokuwa na uwezo wa kuhifadhi na kusambaza lita mil 1.5 za maji kwa wakazi wa Mji huo.
Akizungumza na gazeti hili jana Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo Mhandisi Aidan Ngatomela amesema kukamilika kwa mradi huo kutawezesha wakazi zaidi ya 49,000 wa Mji wa Kibondo kupata huduma ya maji safi na salama hivyo kumaliza kilio chao cha miaka mingi.
Amebainisha kuwa ujenzi wa mradi huo ulioanza mwezi Septemba 2022 kwa sasa umefikia asilimia 59 na unatarajiwa kukamilika Desemba 8 mwaka huu.
Amefafanua kuwa mradi huo ni mkombozi kwa wakazi wa Wilaya hiyo kwa kuwa hadi sasa hawana tenki lolote lenye uwezo wa kuhifadhi na kusambaza kiasi hicho cha maji hali inayopelekea huduma ya maji kusuasua sana katika Mji huo.
‘Tunamshukuru sana Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia kiasi hicho cha fedha ili kutatua kero ya maji kwa wakazi wa Wilaya hiyo,’ amesema.
Mhandisi Aidan ameeleza kuwa wakazi wa Mji huo kwa sasa wanapata huduma kutoka kwenye matenki madogo ambayo hayatoshelezi mahitaji yao hivyo ujio wa mradi huu utasaidia kumaliza kilio chao.
Amebainisha malengo ya mradi huo kuwa ni kuimarisha hali ya upatikanaji huduma ya maji kwa masaa 24 na kutatua changamoto ya upatikanaji huduma hiyo.
Ameeleza changamoto kubwa inayowakabili kuwa ni ukosefu wa tenki lenye uwezo wa kutunza na kusambaza maji ya kutoshelezaji wananchi.
Naye Afisa wa Mamlaka hiyo Mhandisi Glory Dominic amefafanua kuwa ujio wa mradi huoy utawezesha wananchi wengi zaidi kupata maji safi hivyo tatizo la maji katika Wilaya hiyo kubakia historia.
More Stories
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â