November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia, Hichilema waandika ukurasa mpya

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

RAIS Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zambia, wameendelea kuandika ukurasa mpya kwa viongozi wa nchi hizo mbili (Tanzania na Zambia) kukubaliana kuendelea kuondoa vikwazo vya kibiashara na kuweka mazingira wezeshi kwa biashara na uwekezaji kufanyika baina ya mataifa hayo yenye uhusiano wa kihistoria.

Viongozi hao walikubaliana nayo wakati wa kongamano lililowakutanisha wafanyabiashara wa Tanzania na Zambi, juzi nchini Zambia.

Kupitia kongamano hilo, Rais Samia ametumia fursa hiyo kunadi fursa za uwekezaji zilizopo nchini na kuwakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji wa Zambia kuwekeza nchini kwa kuwa Serikali imeweka mazingira wezeshi kwa ajili hiyo.

Amesema Serikali yake inafanya kila linalowezekana kusukuma uchumi na hilo linafanyika kwa kuweka mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji.

Akizungumza kwenye kongamano hilo, Rais Samia amesema; “Serikali ninayoingoza tuna maono ya kutengeneza uchumi imara na shirikishi kwa Watanzania na wote watakaotaka kuja kuwekeza Tanzania.

Ushirikiano huu tunaozidi kuuimarisha kati yetu na Zambia tunaamini utakuwa kichochea katika kusukuma maendeleo ya kiuchumi kwa mataifa yote mawili,” amesema Rais Samia.”

Rais Samia amesema kuwa ziara yake imekuwa na mafanikio makubwa imesaidia kutatua changamoto na vikwazo vinavyowakabili vya wafanyabiashara ambavyo vitapatiwa ufumbuzi.

Ametaja moja ya mafanikio hayo ni kusainiwa kwa MoU sita na mikataba miwili na kwamba katika siku za usoni itasainiwa makubaliano na mikataba mingi zaidi.

Amesema hati za makubaliano zilizosainiwa hapo zikiwemo za serikali na sekta binafsi itaongeza chachu ya kuharakisha maendeleo.

Rais Samia ameishukuru Serikali na watu wa Zambia kwa kumualika katika maadhimisho ya miaka 59 ya uhuru pamoja na kuwashukuru wana Zambia kwa ukarimu wao kwa wageni wote waliotoka Tanzania aliombatana nao.

Kwa upande wake Rais Hichilema amesema hakuna sababu ya mataifa hayo kuweka urasimu na vikwazo katika biashara na uwekezaji kwa kuwa maendeleo yanahitaji kwa kiasi kikubwa ushiriki wa sekta binafsi.

“Nimetoka kwenye sekta binafsi nafahamu hizi nchi zina vikwazo vingi kwenye ufanyaji biashara, ndiyo maana nasema kwa nafasi niliyonayo sasa tuna kila sababu ya kuviondoa hivyo vikwazo, hilo hatuwezi kufanya peke yetu hivyo tumekubaliana na Rais Samia kushirikiana kuviondoa hasa katika eneo la mpakani kwa kuwa sisi ni ndugu hatupaswi kutengenishwa na mikapa,” amesema.

Amesema Serikali katika nchi zote mbili zinapaswa kuondoa vikwazo vinavyoweza kukwamisha biashara, huku akitaka sekta binafsi kuwa sehemu ya jitihada za kukuza uchumi na siyo kuishia kulaumu.

“Sekta binafsi ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi, sasa kama kuna changamoto na hamshiriki katika kuhakikisha zinapatiwa ufumbuzi na kuishia kuilaumu Serikali haiwezi kuwa na tija.”

“Tunataka ushirikiano wetu kwenye uchumi na biashara uzidi kuimarika maradufu kama ilivuo katika uhusiano wetu, hili ndilo linasababisha tunaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha tunaweka mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji,” amesema Hichilema.

Amesema ni muhimu kwa Tanzania na Zambia kuwekeza katika maboresho ya reli ya ushirikiano ya Tazara kwa kuwa ina umuhimu mkubwa katika kukuza biashara baina ya nchi hizo ikitegemewa zaidi kwenye usafirishaji wa bidhaa.

Aidha, miongoni mwa makubaliano ambayo yalifikiwa na viongozi hao ni pamoja na kuondoa urasimu, kuweka mazingira rahisi ya ufanyaji biashara, kuitumia vyema miundombinu inayounganisha nchi hizo na kuruhusu mwingiliano wa watu.

Akizungumzia hatua zinazoendelea kufanyika katika kuweka mazingira bora Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Ashatu Kijaji amesema tangu Agosti mwaka jana baada ya Rais Hichilema kutembelea Tanzania, mawaziri wa kisekta wameshakutana mara kadhaa na wameondoa baadhi ya vikwazo visivyo vya kikodi.

“Kati ya vikwazo 24 tulivyovianisha Serikali zote mbili tayari tumeshaviondoa nane na vilivyosalia tumekubaliana hadi kufikia Desemba 31 mwaka huu tuwe tumevimaliza vyote na vinavyoendelea kuibuka tutavishughulikia hatua kwa hatua.”

“Mimi na waziri mwenzangu wa Biashara upande wa Zambia, tuna vikao kwa njia ya mtandao kila wiki na mara moja kwa mwezi tunakutana katika eneo lenye changamoto iwe ni mpakani au kwenye miji mikubwa ambapo biashara zinafanyika iwe kuanzia au kuishia,” amesema Dkt. Ashatu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (TATOA), Elias Lukumay amepongeza hatua ya Rais Samia kuongozana na wafanyabiashara kwenye nchi ambazo wana uhusiano nao wa kibiashara.

“Hatua hii inatufanya sekta binasi tusijione wanyonge, ni mara kadhaa Rais amekuwa akiongozana na sisi katika nchi za kimkakati ambazo tunafanya nao biashara au tunataka kutengeneza mazungungumzo ya kufungua biashara zetu.”