Na Waandishi Wetu,Timesmajira,Onlibe,Tabora
RAIS Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali kwa miaka miwili na mitatu imeamua kutoa ruzuku kwa wakulima ili kuwapa uwezo wa kufanya shughuli zao za kilimo vizuri, badala ya kutoa fedha zao mkononi na kununua mbegu na pembejeo.
Ametoa kauli hiyo wilayani Igunga wakati akizungumza na wananchi katika Viwanja vya Barafu, ikiwa ni siku yake ya kwanza katika ziara yake mkoani Tabora.
Amesema serikali kwa sasa itatoa mbolea na pembejeo kwa bei nafuu kwa baadhi ya maeneo mengine na maeneo mengine itatoa bure kwa kuwapa wakulima.
“Lengo ni kuwajengea uwezo wakulima, wapate pembejeo na mbolea kwa bei nzuri, Serikali tunaangaika na matokeo ambayo kwa sasa mmeanza kuyaona, mfano mbaazi tumetoka kuuza kwa sh.200 kwa kilo na mwaka huu tumeuza hadi sh. 3,000 kwa kilo katika maeneo tofauti tofauti,”amesema Rais Samia.
Amesema kazi ya Serikali ni kutafuta masoko ya bidhaa zitakazolimwa na pale ambapo masoko ya nje yatakuwa na matatizo, Serikali imejiandaa kununua mazao yote yatakayozalishwa kuweka stoo, huku wakitafuta wanunuaji wa mazao hayo.
Amewaomba kutumia fursa hiyo kujijengea mambo ya baadae.”Ahadi yenu kwenu kazi yetu ni kuwatumikia kila tunapokusanya fedha tunaangalia matatizo ya wananchi yapo wapi na ndipo tunapozielekeza,” alisema.
***Chuo cha VETA
Akizinfua chuo cha Veta, Rais Samia alisema ni muendelezo wa jitihada ya Serikali kuhakikisha vijana wanapata elimu ya amali (ufundi) itakayokwenda kuwasaidia kuajiriwa au kujiajiri.
“Tumeamua wilaya zote za Tanzania kuwa na vyuo vya aina hii, lakini mbali na wilaya kila mkoa kuwa na chuo chake,shabaha yetu ni kujenga vyuo ambavyo vinakwenda kufundisha elimu ya amali kwa vijana wetu na sio nadharia wanazopata shuleni,”amesema na kuongeza;
Amesema vyuo vya VETA vinaenda kufundisha mafundi wa aina zote ili ajira zinapokuja, vijana waweze kujiajiri katika maeneo waliopo.
“Vyuo hivi vinaenda kuangalia mfano Igunga kuna fursa nyingi za kilimo na ufugaji,”amesema na kuongeza;
“Vyuo hivi vinaenda kuzalisha watu mabingwa,mafundi katika masuala ya kilimo na ufugaji ambayo yataleta tija kwa Igunga,”amesema.
Akihitimisha ziara yake mkoani Singida, Dkt. Samia, amesema utekelezwaji wa mradi wa umeme mkoani Singida umefikia asilimia 90 na kuahidi vijiji vyote mkoani humo kupata umeme mwakani
Rais Dkt. Samia, ametoa kauli hiyo alipokuwa akihutubia mkutano uliofanyika wilayani Iramba mkoani Singida.
Rais, Dkt. Samia amesema, Wilaya ya Iramba ni sehemu ya mradi wa (REA) awamu ya tatu mzunguko wa pili, ambao unalenga kufikia vijiji 178 katika Wilaya ya Singida, Singida Vijijini, Ikungi, Manyoni, Mkarama na Iramba.
“Wilaya ya Iramba ni sehemu ya mradi wa REA na hadi hivi sasa mradi wa umeme umefikia asilimia 90 katika ukamilikaji wake na tunatarajia hadi mwaka kesho katikati ya mwaka, Singida yote itakuwa inawaka umeme..ingawa Ilani yetu ya CCM inasema kabla ya mwaka 2025 tuwe tumepeleka umeme nchini kote, lakini kwa Singida maana yake haitafika mwaka huo,” amesema Rais Dkt. Samia.
Amesema Serikali bado inaendelea kuchukua hatua za muda mfupi na za kuimarisha gridi ya Taifa ili kuondoa kero ya umeme kukatika mara kwa mara.
Aidha, aliwahakikishia wananchi wa Singida kuwa Serikali ipo makini ili kuhakikisha inatekeleza ahadi zote zilizotolewa wakati wa kuomba dhamana ya kuingiza Taifa kupitia chama cha CCM na kuzichukua changamoto na mahitaji ya maendeleo, ambayo mengi yanapitia kwenye mikono ya Tamisemi.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa