November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NSSF ni wadau muhimu kwa vijana – Masha Mshomba

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Masha Mshomba, amepongeza hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuwawezesha na kuwainua vijana kupata fursa mbalimbali za ajira.

Mshomba amesema hayo tarehe 13 Oktoba 2023, wakati alipotembelea Maonesho ya Wiki ya Vijana yanayofanyika katika Stendi ya Zamani, Babati Mkoani Manyara, akiwa amefuatana na Mkurugenzi wa Uendeshaji wa NSSF, Omar Mziya na Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Ndani, Godfrey Ngonyani.

Amempongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi nzuri anayoifanya katika kuhakikisha vijana wanashiriki shughuli mbalimbali za kiuchumi.

“Namtakia kila la heri Mheshimiwa Rais katika kuhakikisha malengo yake aliyonayo kwa vijana na Watanzania kwa ujumla yanatimia na nchi yetu inapiga hatua za maendeleo,” amesema Mshomba.

Mshomba amesema vijana ni wadau muhimu kwa NSSF kwa sababu ndio nguvu kazi kubwa ya Taifa, na pia ni wanachama wa Mfuko, ambapo baadhi wanachangia kupitia sekta binafsi na wengine wanachangia kupitia sekta isiyo rasmi.

“Ushiriki wa NSSF katika Maonesho haya ya Wiki ya Vijana umewalenga moja kwa moja vijana ambao tunawapatia elimu ya hifadhi ya jamii ili waweze kujiunga na kujiwekea akiba kwa maisha yao ya sasa na ya baadaye,” amesema Mshomba.

Amesema suala la hifadhi ya jamii ni muhimu kwa sababu linatoa uhakika wa maisha ya binadamu hasa baada ya uwezo wake wa kufanyakazi kupungua ambapo NSSF itaweza kumlipa mafao yakiwemo ya uzee.

Mshomba ametoa wito kwa wananchi wakiwemo vijana kujiunga na kuchangia kwa wingi ili kuandaa kesho yao iliyokuwa njema.

Ametumia fursa hiyo kuipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa jinsi walivyojipanga vizuri na kufanikisha vizuri maadhimisho hayo.

Vilevile, Mshomba ameipongeza Bodi ya Wadhamini kwa miongozo wanayotoa kwa NSSF pia wafanyakazi kwa kazi nzuri wanazofanya.

Amesema NSSF iko imara na mpango wa uchangiaji wa sekta isiyo rasmi uko imara na lengo ni kuhakikisha inawafikia wananchi wengi zaidi kupata elimu ya hifadhi ya jamii pamoja kuwaandikisha kwa ajili ya kujiwekea akiba.

Matukio mbalimbali katika picha