November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Benjamin Mkapa yajihakikishia kupata Division one 150

Na Heri Shaaban, TimesMajira Online

SHULE ya Sekondari ya Benjamin Mkapa iliyopo katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imesema inajivunia maendeleo ya kitaaluma kwa mitihani ya taifa ya kidato cha nne na sita huku ikitarajia kufaulisha kwa kupata divison one 150 mwaka huu.

Akizungumza jana wakati wa mahafali ya kidato cha nne Mkuu wa Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Joseph Deo, amesema mwaka jana wanafunzi 102 walipata daraja la kwanza katika mtihani wa kitado cha nne.

Amesema mwaka 2022 ufaulu wa kidato cha nne ulikuwa asilimia 96, mwaka 2021 asilimia 97 na mwaka 2022 asilimia 97.

Kwa upande wa matokeo ya kidato cha sita amesema mwaka 2021 ufaulu ulikuwa asilimia 100, mwaka 2022 asilimia 99 na mwaka 2023 asilimia 99.

“Kwa matokeo ya kidato cha nne mwaka jana shule ilifanikiwa kupata wanafunzi wenye ufaulu daraja la kwanza 102, hili ni jambo kubwa wa shule yetu na la kujivunia. Tunaamini kwa jitihada za walimu na wanafunzi mwaka huu tutapunguza ‘division zero’ ikiwezekana kupata ‘division one’ 150 au zaidi, tunaweza,” amesema Deo.

Amesema nidhamu ya wanafunzi wa shule hiyo ni nzuri kutokana na ushirikiano uliopo kati ya walimu, wafanyakazi pamoja na wazazi na wanafunzi ambayo imekuwa kichocheo kikubwa kwa maendeleo mazuri ya kitaaluma.

Amesema pia wamefanikiwa kutoa wachezaji wawili wa mpira wa miguu katika timu ya taifa chini ya miaka 17 iliyoshiriki mashindano ya Afrika nchini Ethiopia.

“Wachezaji wawili wa kikapu wapo timu ya taifa ‘under’ 20 iliyoshiriki mshindano ya Afrika Mashariki yaliyofanyika Rwanda mwaka huu. Shule yetu pia imefanikiwa kutoa mwanafunzi mmoja wa mchezo wa kikapu kwenda kusoma Marekani na kucheza ‘basketball’,” amesema.

Deo pia amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza ahadi yake ya kutatua changamoto za shule hiyo ambapo tayari ujenzi wa ukumbi, maktaba na uwanja kwa kuweka nyasi bandia unaendelea.

Kwa upande wake mgeni rasmi katika mahafali hayo ambaye ni Mkurugenzi wa Zamaradi Media, Zamaradi Mketema, ameahidi kuwahudumia wanafunzi wawili wanaoishi kwenye mazingira magumu kwa kipindi chote cha masomo yao.

Wanafunzi hao mmoja ni yatima na mwingine ni kiziwi ambaye aliacha shule kutokana na kushindwa kumudu gharama za nauli na chakula na wote wanasoma kidato cha kwanza.

Aidha kupitia mfuko ulioanzishwa na wanafunzi hao kwa ajili ya kuwasaidia wenzao wenye changamoto mbalimbali (Charity Group Foundation), Zamaradi pia alichangia Sh 500,000 kwa kula keki ili kutunisha mfuko huo.

Katika mahafali hayo wanafunzi 254 walihitimu kidato cha nne na baadhi yao walizawadiwa kwa kufanya vizuri katika maeneo mbalimbali.