November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Benki ya KCB yakabidhi madawati 120 Jimbo la Kibaha Mjini

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Banki Ya KCB imekabidhi Madawati 120 katika shule tano za msingi jimboni Kibaha mjini yenye thamani ya shilingi milioni 24

Hii ni kutokana na upungufu wa madawati 3516 kwa wanafunzi wa shule hizo.

Akizungumza juzi wakati wa hafla fupi ya ugawaji wa madawati hayo
Mkuu wa Masoko, uhusiano na Mawasiliano kutoka Benki ya KCB, Christina Manyeye alisema madawati hayo yataenda kusaidia wanafunzi 360 kwa awamu ya kwanza.

“Leo Benki ya KCB tuko hapa katika Jimbo la Kibaha kukabidhi madawati katika shule tano ambapo msaada huu utakua ni endelevu “

Manyeye alisema wao kama KCB wanaendelea na juhudi zao za kusaidia Sekta ya elimu, afya na mazingira ambapo hadi sasa wanafunzi vijana 2000 tayari wamepelekwa shule na wengine 4400 wataingia kati ya sasa na mwaka ujao.

Kwa upande wake Afisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya Kibaha Benedina Kahabuka alisema kuwa katika Halmashauri hiyo wana wanafunzi 42, 516 ambao si wote wana madawati ya kutosha hivyo aliwashukuru Benki ya KCB kwa msaada huo ambao utaenda kupunguza adha ya upungufu wa madawati.

“Tunamshukuru Mbunge wetu kwa kutuletea wafadhili hawa ambao wametuletea madawati haya 120 katika Jimbo letu ambayo ni sapoti kubwa kwa serikali, Halmashauri na mwanafunzi mmoja mmoja kwani haendi tena kukaa chini”

“Jimbo la Kibaha kupitia mapato ya ndani na serikali tunaendelea kupunguza wimbi la changamoto la madawati mashuleni hivyo tunawashukuru KCB kwa mchango huo wa madawati ” Alisema

Mbunge wa kibaha mjini Sylvestry Koka, alisema utunzaji wa madawati hayo ndiyo itawafanya kuendelea kutatua changamoto walizonazo za madawati hatua kwa hatua.

Pia alisema wanapeleka madawati 40 katika shule ya Msingi Mkuza ambapo wanafunzi 120 watapata sehemu ya kukaa, madawati 20 katika shule ya msingi Miembe Saba ambapo wanafunzi 60 watapata sehemu ya kukaa, madawati 20 katika Shule ya msingi Maendeleo sawa na wanafunzi 60 watapata sehemu ya kukaa, madawati 20 katika shule ya msingi Kidimu sawa na wanafunzi 60, na madawiti 20 shule ya msingi Kambarage.

“Tunawashukuru sana Benki ya KCB Kwa kupokea ombi letu na kulifanyia kazi iliyo njema na yenye kiwango

Alisema bado mahitaji ya madawati ni makubwa hivyo aliiomba serikali kuendelea kuwaunga mkono kutatua changamoto hiyo.

Nao baadhi ya Wanafunzi wa Shule hizo waliishukuru Benki ya KGB kwa kuwapatia msaada huo kwani itawasaidia kujifunza katika mazingira Bora.

Mkuu wa Masoko, Mawasiliano na Uhusiano wa KCB Bank Christina Manyenye akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji akimkabidhi madawati 120 Mbunge wa Kibaha Mjini, Sylvestry Koka ambayo yataenda kusaidia Shule tano za Msingi katika Wilaya ya Kibaha Mjini. Kulia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kibaha Mjini Mhandisi Msham Munde na Meneja Uhusiano wa Wateja wa Kubwa wa KCB Bank, Clara Sannda (kushoto).