Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko amezindua mpango mkakati wa kutangaza fursa zilizopo katika Sekta ya Utalii katika wilaya ya Pangani, mkoani Tanga ili kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuikuza sekta hiyo nchini.
Dkt. Biteko alifanya uzinduzi huo Oktoba 7, 2023 jijini Dar es salaam katika Kongamano la Uwekezaji la Swahili International Tourism Expo lenye lengo la kutangaza fursa za uwekezaji zilizoko katika wilaya hiyo ikiwemo utalii katika mbuga ya Saadani, fukwe, kilimo biashara pamoja na uchumi wa Buluu katika wilaya hiyo.
Ambapo Dkt. Biteko aliwataka viongozi wote wa serikalini kwenda kufanyia kazi na kutekeleza kusudio hilo la Rais Dkt. Samia la kukuza utalii ndani ya nchi ili utalii uwe mbadala wa kuleta fedha za kigeni, kukuza uchumi lakini pia kuongeza ajira.
“Rais Dkt. Samia amekuwa kinara wa kutangaza utalii wa nchi, hivyo kazi hiyo hawezi kuifanya pekeyake hivyo ni wajibu wa wote waliopo kwenye nafasi mbalimbali ngazi za wilaya, mikoa, Taasisi za serikali,wakala zinazojitegemea kuungana kuunga mkono juhudi za Rais Samia za kutangaza utalii ili utalii uwe mbadala wa kuleta fedha za kigeni na kukuza uchumi lakini pia kuongeza ajira”
“Mambo hayo hayawezi kutokea kama wananchi wote tutamuachia Rais Samia pekeyake abuni na kufanya juhuzi za kutangaza utalii kwani tutakua tunamchelewesha”
Aliwataka viongozi hao pia kwenda kuwahudumia na kuwasikiliza watanzania walioko mbali na makao makuu ya Wilaya, vijijini na wale wanaotegemea Mipango ya serikali kwaajiii ya kujiondolea umasikini, kwa kuwasaidia ili watoke kwenye umasiki na wawe na maisha bora
“Rais Samia anajenga miundombinu ya kuwaletea maendeleo watu wake, hivyo tutumie fursa hii ya kuwasaidia watanzania kuwaondoa kwenye umasikini, Kila mtu mahali pale atimize wajibu wake, asisubili atumwe bali ajitume”
Vile vile, alisisitiza kuwa, Kongamano hilo litumike kuitangaza wilaya ya Pangani na kubadilishana mawasiliano ili fursa zilizoko Pangani ambazo hazipatikani kwengine zishawishi watu wengine kuzifuata.
“Niwapongeze sana watu wa Pangani kupitia Mkuu wa wilaya kwa ubunifu huu wa hali ya juu na nitoe wito kwa wilaya zingine kuiga Pangani na kufungua fursa za utalii na uwekezaji kwenye wilaya zao” Alisema Dkt. Biteko.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Dunstan Kitandula alisema kuwa, sekta ya utalii kwa sasa mchango wake katika Pato la Taifa ni asilimia 17. Alisema Serikali itaendelea kuboresha mazingira rafiki katika sekta hiyo ili kuendelea kuvutia utalii nchini katika maeneo mbalimbali hususan wilaya ya Pangani.
Mkurugenzi idara ya uhamasishaji uwekezaji kituo cha uwekezaji Tanzania -TIC,John Mnali alisema Serikali imejipanga vizuri kuhakikisha kwamba wawekezaji wote watakaokuja kuwekeza pangani wanapata usaidizi wa kupata vibali na leseni mbalimbali watakazozihitaji kupitia huduma za mahali pamoja ambazo ziko katika kituo Cha uwekezaji na Mamlaka ya uzalishaji kwaajili ya mauzo ya nje
Hivyo aliwataka wawekezaji kuchangamkia fursa katika sekta za Utalii, viwanda, kilimo na uvuvi ambazo hupatikana wilayani Pagani Mkoani Tanga.
Awali akizungumza kabla ya mgeni rasmi, Mkuu wa wilaya ya Pangani Zainabu Abdallah alisema, wilaya ya Pangani imejikita kwenye uwekezaji wa maeneo matatu ikihusisha utalii , kilimo mkakati na uchumi wa bluu na kuongeza kuwa wilaya hiyo ni miongoni mwa wilaya ya kimkakati yenye mazingira mazuri ya uwekezaji.
” Serikali imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji na tunawaomba wawekezaji kufika wilaya ya pangani kujionea fursa hizo muhimu “alisisitiza Zainabu
Uzinduzi wa mpango huo ulikwenda sambamba na Kongamano la uwekezaji chini ya maonyesho ya wadau wa Sekta ya Utalii kuunga mkono fursa za uwekezaji.
Wengine walioshiriki hafla hiyo ni Viongozi mbalimbali wa Serikali, watendaji wa taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo na wadau wa sekta ndani na nje ya nchi.
More Stories
Mzumbe yaanika siri ya shahada udaktari wa heshima kwa Samia
Kujenga ofisi ya kisasa,akipewa ridhaa ya Uenyekiti
Ushiriki wa Rais Samia G20 wainufaisha Tanzania