November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia kufanya ziara nchini India

Na Irene Clemence, TimesMajira Online

RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajia kufanya ziara ya siku tatu nchini India kuanzia Oktoba 8 hadi 11 mwaka huu kwa mwaliko wa viongozi wa nchi hiyo

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, January Makamba, amesema madhumuni ya ziara hiyo ya Rais Dkt. Samia imelenga kuimarisha na kudumisha uhusiano uliokuwepo muda mrefu kati ya nchi hizo mbili.

Amesema uhusiano huo wa muda mrefu ulijikita hasa katika sekta za kimkakati , viwanda, afya, elimu, biashara, ulinzi na usalama, uchumi wa blue, sekta ya maji, pamoja na sekta ya kilimo.

Waziri Makamba alisema ziara hiyo pia imelenga kutafuta fursa za kibiashara kati ya Tanzania na India pamoja na kivutia wawekezaji na wafanyabiashara kutoka India na kuja kuwekeza hapa nchini

“Kama mnavyofahamu nchi yetu sisi inatafuta maendeleo na moja ya chanzo cha maendeleo hayo ni biashara na uwekezaji na India ni nchi kubwa na yenye uchumi mkubwa na mtaji mkubwa.

Hivyo Rais anachokwenda kuongeza ushawishi ili wawekezaji na wafanyabiashara kutoka India waje kuwekeza nchini pamoja na kuendeleza na kukuza biashara inayokuwa kwa kasi kati ya nchi hizi mbili,”alisema Waziri Makamba

Waziri Makamba amesema yapo matarajio ya ziara hiyo ambayo yatawawezesha Watanzania kupata fursa ya mafunzo katika nyanja mbalimbali nchini India ukiacha zinazoendelea wa sasa katika mafunzo

Amesema ziara hiyo itazaa nafasi 1,000 za papo kwa papo katika mafunzo katika sekta mbalimbali kutokana na nchi India kuingiza katika mapinduzi ya kidigitali, hivyo mategemeo ya ziara viwanda na wawekezaji kuja kuwekeza nchini ikiwemo viwanda vya kutengeneza simu

Pia amesema nchi ya India ina mafanikio makubwa katika huduma ya afya, hivyo ziara hiyo itakwenda kupanua na kukuza uhusiano katika sekta hiyo.