Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
WATEJA wa Benki ya Biashara ya Mwalimu (MCB), wameitaka benki yao kujitangaza zaidi na kuwafuata wateja walipo ili nao wanufaike na huduma bora za benki hiyo.
Wakizungumza na uongozi wa MCB, wakati wa maadhimisho ya wiki ya Huduma kwa Wateja, iliyofanyika na jijini Dar es Salaam leo Oktoba 4,2023 walisema huduma bora za benki hiyo zinastahili kuwafikia watanzania wote.
Mwalimu Ashura Masoli kutoka Shule ya Msingi Uhuru Wasichana, alisema walimu wengi wanatamani kujiunga na benki hiyo ambayo kimsingi ni mali yao ila wanakosa taarifa sahihi na hamasa kutoka kwa watumishi wa MCB.
“Tunawaomba mtoke ofisini, njoeni mtaani, shuleni, vyuoni tembeeni msikae tu wateja wanatafutwa, wanashawishiwa fanyeni kama wengine hii ni taasisi kubwa sana ongezeni nguvu kupambana na waliofanikiwa sana kwenye sekta hii,” alisema Masoli ambaye pia ni mwanahisa wa MCB.
Kwa niaba ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Mwalimu (MCB), Richard Makungwa, Mkuu wa Idara ya Huduma na Teknolojia, Abdallah Kirungi, amesema benki hiyo inaendelea kuboresha huduma zake kidijitali zaidi.
Kirungi amesema inaendelea kujiweka karibu zaidi na wateja wake kwa kuhakikisha inaboresha huduma zake kidijitali na weledi.
“Hii ni siku muhimu kwa wadau wetu hapa ni mahala sahihi kwetu kuendelea kuwahakikishia usalama na uhakika wa huduma zetu, ninyi ni nguzo yetu, hatuna budi kuja kwenu na kuwapa uthibitisho wa hatuza za maendeleo ya benki yenu na usalama wa fedha zenu.
“Kaulimbiu ya siku ya huduma kwa wateja mwaka huu, inasema Team Service nasi tunawahakikishia kuwa ni timu inayowafikia mlipo, leo watumishi wa MCB wapo kituo cha basi Mbezi Mwisho hii ni katika kuwafuata wateja wetu walipo… tunawaahidi kufika kila mahali,” alisema Kirungi.
Kwa mujibu wa Kirungi, MCB imewashukuru wateja, wadau na wafanyakazi wake kwa mchango mkubwa katika uhai wa benki hii katika kipindi hiki cha miaka saba tangu kuanzishwa kwake.
Amesisitza kuwa MCB imefanikiwa kuongeza idadi ya ofisi za kutolea huduma katika mikoa nane, mawakala wa huduma na kuboresha huduma za kibenki kwa njia za simu za mkononi na kadi ya MwalimuCard Visa.
Hii imewezesha wateja kufanya malipo mtandaoni, kulipa kupitia mashine za POS na kutoa pesa kupitia ATM zenye huduma za Visa zaidi ya 1500.
Ili kufikia lengo la kuwagusa wateja wanawake na wafanyabiashara wadogo na wa kati, MCB imezindua bidhaa mpya mbili yaani akaunti ya Tunu na akaunti ya Mtaji.
Akaunti hizi mbili ni mageuzi makubwa katika huduma za kibenki ambapo kupitia akaunti ya Tunu wanawake wenye malengo ya kujiwekea akiba na wanaojihusisha na biashara na ujasiriamali wanasimamiwa na kuongozwa katika kufikia kilele cha mafanikio kulingana na matarajio yao, huku wakijipatia faida kila mwezi kwa fedha iliyowekwa.
Huduma hii inaruhusu wateja kuchagua utaratibu wa kiwango wakati wa kujiwekea akiba na kutoa fursa ya kupata mkopo wa dharura wa hadi asilimia 95 ya akiba, huu ni mwendo wa mageuzi makubwa sana kwenye sekta ya kibenki kupitia MCB.
Kwa upande mwingine akaunti ya mtaji hutoa fursa maalumu kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati kukuza shughuli zao za kibiashara, akaunti hii inaruhusu wateja kuweka, kupokea fedha, kufanya malipo, kupokea malipo, kutoa na kuweka standing order na kupata mkopo.
Kiungi amesema, MCB itaendelea kutoa huduma bunifu za kifedha kwa uwajibikaji, usawa, uhakika, uwazi, usiri na usalama mkubwa kwa wateja wake na kusisitiza kwamba ni benki yenye riba ndogo kuliko zote.
More Stories
DC Mgomi ataka wahitimu Jeshi la Akiba kuwa macho ya Serikali
Viongozi,Makada CCM kufanya ufunguzi kampeni Serikali za Mitaa
Wadau wachangia vifaa Kariakoo