November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kesi ya Kisena, wenzake ngoma nzito

Na Irene Fundi, TimesMajira Online

KESI ya kulisababishia hasara ya sh. bilioni 14 Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) inayowakabili wafanyabiashara watatu, akiwmo mfanyabiashara maarufu jijini Dar es Salaam, William Kisena (44) imeahirishwa kutokana na kutokamilika kwa upelelezi.

Wakili wa Serikali, Fatuma Waziri amedai hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate, wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

Mbali na Kisena, washtakiwa wengine ambapi pia ni wafanyabiashara ni Saimon Bulenganija (43) na Leonard Lubuye .

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Kabate ameahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 16, 2023 kwa ajili ya kutajwa.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka inadaiwa kuwa washtakiwa walitenda kosa hilo Oktoba Mosi, 2011 ambapo walighushi mkataba wa uongo wa kukodisha eneo baina ya UDA na Kampuni ya Simon Group Limited,kwa gharama ya sh milioni 400 kwa mwaka ndani ya miaka 10, katika eneo lililipo Kurasini lenye ekeri 13, wakati wakijua kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.

Katika shtaka pili la utakatishaji fedha inadaiwa kuwa Desemba 2018 katika jiji la Dar es Salaam washtakiwa wote walijipatia sh bilioni 14 kutoka UDA wakati wakijua fedha hizo zinatokana na kosa la kwanza la kughushi.

Katika shtaka la tatu la kuisababishia hasara Mamlaka hiyo, inadaiwa kuwa washtakiwa wote Mei, Mosi, 2011 na Desemba 12, 2022 , kwa nia ovu walijipatia fedha sh. bilioni 14 na kusababisha shirika hilo kupata hasara.