November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Majinge aunga mkono kauli ya Rais Samia kuhusu elimu ya Katiba

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Msaikososholojia na Mtaalam wa Maendeleo ya Binadamu na Afya ya Akili Kinga, Dkt Mayrose Majinge ameunga mkono kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhusu wazo la kuwapa wananchi elimu ya Katiba .

Amesema kuna haja kubwa ya kutoa elimu kwa watanzania kuelewa maana ya Katiba, kujulishwa maana ya uzalendo na vipi upatikana katika nchi lakini pia kuelezwa kuhusu Mamlaka ya Rais.

Dkt. Majinge ameyasema hayo Juzi Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa Habari kuhusu katiba ya nchi, uzalendo na suala la kuongeza au kupunguza Mamlaka ya Rais.

Amesema Mambo hayo matatu yakieleweka vizuri Taifa litakuwa limejiwekea mazingira mazuri ya kupata katiba madhubuti itakayosaidia kujenga Taifa madhubuti.

“Kwa mujibu wa taaluma ya maendeleo ya Binadamu nashauri kwamba ikiwa hatutazingatia kutoa elimu kuhusu maeneo haya matatu niliyoyaainisha nashauri tusitishe mchakato mzima ama kurekebisha au kuandaa katiba mpya ya kisasa”

Aidha ametoa rai kuhusu mchakato wa katiba mpya ambapo amesema kabla hawajaanza mchakato wa kukamilisha katiba mpya ni muhimu wakajikita katika kuimarisha katiba ya kimapokeo lengo ikiwa ni kupata katiba ya nchi iliyo madhubuti kwa vizazi na vizazi.

Kuhusu suala la kupunguza au kuongeza Mamlaka ya Rais, Dkt. Majinge amesema haipaswi kumpunguzia Mamlaka Wala madaraka Rais bali iwe kuimarisha Mamlaka na madaraka ya Taasisi ya Urais kwani Rais ni Taasisi.

“Hii inapelekea kujenga Taifa lenye nguvu kwani tunajihakikishia muundo wa mfumo wa jamii yenye uzalendo na hivyo tunalutengenezea Taifa matokeo chanya ya mwisho tarajiwa kwa maendeleo endelevu ya watanzania wa kizazi na kizazi”

Kwa upande wa uzalendo na namna unavyopatikana katika nchi amesema kwa mujibu wa wataalamu wa Maendeleo ya Binadamu, uzalendo katika Taifa lolote unatokana na uimara wa katiba ya kimapokeo na namna Taifa litakavyoenzi hadhi, heshima na ustawi wa wazee wastaafu wa Taifa husika katika maisha yao yote.

Hivyo Dkt. Majinge amesema katiba ya nchi na uzalendo ndiyo muhimili wa Maendeleo endelevu ya nchi.