Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
WAKALA wa Elimu ya Vyuo Vikuu Nje ya Nchi, Global Education Link (GEL), imewataka wazazi ambao watoto wao wamekosa nafasi za kusoma vyuo vikuu ndani ya nchi wasipate mfadhaiko wa moyo na badala yake wafike GEL kwaajili ya kupata nafasi kwenye vyuo vikuu nje ya nchi ndani ya muda mfupi.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa GEL, Abdlulmalik Mollel, wakati akizungumza na wazazi na wanafunzi zaidi ya 100 ambao wanatarajia kusafiri wiki hii kwenda nje ya nchi kuanza mwaka wa masomo.
Amesema wanafunzi hao walielezwa mambo ya msingi ya kuzingatia kabla ya safari, wakati wa safari na hata baada ya kufika kwenye nchi wanazokwenda hasa kuzingatia masomo na kuachana na biashara zingine ambazo zitawapotezea malengo.
Amesema anafahamu kwamba wanafunzi wengi wanaotaka kusomea fani za uhandisi na udaktari wamekosa nafasi kutokana na ushindani mkubwa uliokuwepo kwenye vyuo vya ndani lakini hawana sababu ya kupata presha kwani nafasi bado zipo kwenye vyuo mbalimbali nje ya nchi.
“Tunafahamu kwamba wanafunzi wengi hasa wa masomo ya uhandisi na fani za afya kama udaktari wamekosa kwasabahu nafasi ilikuwa chache kwa hapa nchini lakini njooni Global Education Link tutahakikisha watoto wenu wanapata nafasi ndani ya muda mfupi uliobaki na watasafiri kwenda kusoma,” vyuo mbali mbali nje ya nchi,” amesema
Aidha, Mollel amesema mbali na kuunganishwa na vyuo vikuu nje ya nchi kwa haraka kwenye mwaka huu wa masomo, wanafunzi ambao watapata changamoto ya ada watapatiwa mikopo isiyo na riba kwaajili ya ada ili wawahi mwaka wa masomo.
“Wazazi mliobahatika kuja hapa leo tunaomba muendelee kutuamini lakini pia muwatangazie wazazi wengi ambao watoto wao wamekosa nafasi za vyuo vikuu Tanzania kwamba ndoto za watoto wao zinaweza kutimia kwani nafasi zipo, waje kwetu tutawapa Visa na tiketi ndani ya muda mfupi, wasikae kinyonge wakadhani watoto wao wamekwama kabisa,” amesema
“Wazazi lazima watambue kwamba mtoto wako anaweza kuwa amepata daraja la kwanza lakini anazidiwa point na wenzake waliochukuliwa kwenye vyuo vya hapa nchini lakini hiyo haimaanishi kwamba amefeli, amekosa nafasi kutokana na ushindani uliokuwepo kwa hiyo njooni GEL tuwaunganishe na vyuo vya nje ya nchi nafasi bado zipo wataenda kusoma,” amesema Mollel
Amewataka wanafunzi wa vyuo vikuu ni watu wazima wanaotakiwa kuanza kutatua changamoto watakazokutana nazo kwa kuwasiliana na maofisa wa vyuo vikuu walivyopo au maofisa wa Global na kuachana na kasumba ya kuwasumbua wazazi wao kwa kila jambo ambalo wanaona haliko sawa.
“Unakuta mwanafunzi kaona mende chumbani kwake anapiga picha anamrushia mzazi wake sasa unataka mzazi wako atasafiri kuja China kuondoa mende? Ukiwa mwanafunzi wa chuo kikuu ni mtu mzima unayeweza kukabiliana na changamoto kwa hiyo siyo kila kitu unamwambia mzazi wako. Kama umekuta chumba ni kichafu safisha, kama umekuta mende muondoe mende siyo unamwambia mzazi wako,” amesema Mollel.
Amesema kwa mwaka huu wa masomo Global Education Link inatarajia kusafirisha zaidi ya wanafunzi 1,500 kwenda kusoma vyuo vikuu mbalimbali nje ya nchi na kuahidi kuwa wengine watakaojitokeza watapatiwa nafasi za kwenda kwenye vyuo vikuu mbalimbali kwani ushindani vyuo vya ndani umekuwa mkubwa na wengi wao wamekosa nafasi.
“Udahili wa vyuo vikuu vya ndani umefikia ukingoni, dirisha la pili limefungwa dirisha la tatu litafungwa tarehe 29 mwezi huu inawezekana kukawa na kundi kubwa linataka kusomea udaktari wa meno, moyo, mama cheza au zozote zile kama uhandisi kama kuna mwanafunzi amekosa kozi ya yoyote ya sayansi mwanafunzi asihisi amechelewa aje Global au apige simu hii 0656200200 atapata nafasi nje ya nchi,” amesema
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa