November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia kuandika rekodi ya Royal Tour

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Kilimanjaro

FILAMU ya Royo Tour ambayo Rais Samia Suluhu Hassan, alishiriki kwa lengo la kutangaza vivutio vya utalii nchini, itawezesha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Kilimanjaro (KIA) kupata watalii milioni moja kwa mwaka na zaidi ya asilimia 80 kwa mara ya kwanza.

Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Hassan Chande, alipotembelea na kufanya ukaguzi kwenye kituo cha forodha kilichopo katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Kilimanjaro (KIA) wakati akihitimisha ziara yake ya siku mbili mkoani Kilimanjaro.

“Rais Samia katika filamu ya Royal Tour, amesaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza idadi ya watalii ambapo kupitia Uwanja wa Ndege wa KIA, inategemea kupata zaidi ya watalii milioni moja kwa mwaka sawa na zaidi ya asilimia 80 kwa mara ya kwanza,” alisema Chande.

Alisema haitakuwa vyema wageni wa idadi hii wakute changamoto ya foleni kwa sababu ya changamoto ya mdaki, tutaliweka sawa kwa haraka ili wakitoka KIA wawe mabalozi wazuri kuhusu huduma wanazozitoa.

Kutokana na sababu hiyo, Chande aliahidi kwamba Serikali itaboresha vituo vya Forodha mkoani Kilimanjaro, kwa kuweka vifaa vya kisasa, kuboresha majengo ya ofisi hasa jengo upande wa mizigo (Cargo), kuboresha mazingira ya nyumba za watumishi wa kituo hicho na kuongeza vitendea kazi kama vile mdaki. (Scanner kwa upande wa wageni wanaowasili.

Aliahidi kufanyia kazi changamoto ya vitendea kazi, ikiwemo Midaki (Scanners).

Chande alisema ndani ya mwaka huu wa fedha 2023/24, Serikali itahakikisha inaweka kipaumbele kuwapatia Mdaki (Scanner) moja katika kituo hicho cha Forodha cha KIA ili kuongeza ufanisi wa ukusanyaji mapayo ya Serikali.

“Katika ziara hii nimetembezwa kuona sehemu zenye changamoto na naahidi kuwa Serikali itafanyia kazi hasa katika kupata mdaki (Scanner) mpya, na vituo vyote vya forodha nilivyotembelea tumeona hii changamoto na Serikali itahakikisha inalitatua” Alisema Mhe. Chande

Aidha, Chande aliwaomba watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kufanya kazi kwa uadilifu ili kukuza ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha huduma wanazotoa kwa walipa kodi iwe ya wazi na kwa uzalendo.

Pia amewaahidi kuboresha mazingira yao ya kazi kwa kuboresha makazi yao yaliyopo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), ile wakaze katika mazingira yanayokidhi utoaji wa huduma bora kwa wateja.

Naye Afisa Mfawidhi kutoka TRA- Kituo cha Forodha cha KIA, Pius Marwa, alisema kuwa kama ilivyo kwa vituo vingine vya Forodha vya Mamlaka ya Mapato Tanzania, Kituo cha Forodha KIA, kina jukumu la msingi la kuendelea kusimamia na kudhibiti mapato ya Serikali kwa mizigo inayotoka na kuingia ndani ya nchi kupitia KIA. Na hii hufanyika kwa mujibu wa Sheria na taratibu za Nchi.

Marwa aliongeza kuwa, Kituo cha Forodha cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Kilimanjaro (KIA) kilipewa lengo la kukusanya sh. bilioni 15.2 kwa mwaka wa Fedha 2020/2023, ambapo kilifanikiwa kukusanya kiasi cha Shilingi bilioni 16.9 ikiwa ni sawa na asilimia 111.17% ya lengo.

“Mafanikio haya yamepatikana kwa juhudi kubwa za Serikali na Menejimenti ya TRA kuanzia ngazi ya mkoa hadi Makao Makuu, pamoja na ushirikishano wa walipa kodi, utumiaji wa mifumo ya Kielektroniki na ubunifu wa watumishi kwa ujumla” alisema Bw. Marwa.

Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Amiri Mohammed Mkalipa, alimuahidi Naibu Waziri wa Fedha kuwa, watafanyiakazi maagizo yaliyotolewa na kuhakikisha wanaboresha Miundombinu ya barabara (PHASE II) pamoja na  maeneo ya ukusanyaji wa mapato ya forodha.

Chande amehitimisha ziara hiyo mkoani humo ambapo alitembelea Vituo vya Forodha vya Tarakea na Holili na kufanya mkutano na wafanyabiashara ili kujua changamoto mbalimbali wanazopitia wafanyabiashara mkoani humo na kuhamasisha matumizi sahihi ya mashine za Kieletroniki (EFD).