December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

ATARE: Maendeleo hupatikana kwa kufanya tafiti

Na Mwandishi wetu Timesmajira Online


CHAMA Cha Watafiti Tanzania (ATARE),kimesema hakuna nchi yoyote duniani iliyopata maendeleo bila ya kufanya tafiti hivyo ni muhimu kuwekeza katika eneo hilo.

Hayo yamebainishwa jijini Dar es salaam na Rais wa ATARE ambaye pia ni Mwanzilishi wa Chama hicho ,Profesa Joseph Ndunguru wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utendaji wa Chama hicho.

“Tunapoongelea uchumi wa viwanda lazima kuwe na utafiti ambao unalenga kuboresha bidhaa zinazozalishwa viwanda,”alisema Profesa Ndunguru.

Amesema utafiti ni kitu muhimu katika maendeleo ya nchi kwasababu kupitia tafiti kunaweza kuleta suluhu ya mambo mbalimbali ikiwemo kutibu magonjwa mbalimbali.

Aliongeza kuwa malengo mahususi ya chama hicho ni kuanzisha ushirikiano ambao itaisaidia wanachama wake katika kuanzisha na kuendeleza mipango mbalimbali ya utafiti.

“Ili uweze kuwa mtafiti mzuri ni lazima ushirikiano na Watafiti wengine nje na ndani ya nchi hivyo Chama hiki kitakuwa kinasaidia kuratibu,”alisisitiza Profesa Ndunguru.

Aliendelea kueleza kuwa Chama hicho kitaamasisha ufanyanyaji wa tafiti za kisayansi na kuongeza usambazaji taarifa na maarifa kwa maendeleo endelevu.

Vilevile amesema kupitia Chama hicho kutaanzishwa mfuko wa Rasilimari fedha zitakazotoka katika vyanzo mbalimbali kwa ajili ya kusaidia miradi ya tafiti kwa wanachama wake.

“Utafiti unahitaji fedha nyingi na mara nyingi Serikali pekee yake haiwezi kutafutia fedha za kutosheleza utafiti hivyo kupitia Chama hiki tutakitumia kutafuta vyanzo vya fedha kwa ajili ya wanachama wake ili waweze kuendeleza tafiti zao,”amesema Profesa Ndunguru.

Hata hivyo amesema ATARE itakuwa na utaratibu wa kuwajengea uwezo watafiti vijana na wanawake na wanaoibukia katika fani hiyo ili kukabiliana na changamoto mbalimbali.

Aidha alitoa wito kwa watafiti kujiunga na Chama hicho ili waweze kukuza uchumi wa nchi kupitia tafiti.

“Hiki ni Chama cha kwanza cha Watafiti na wazo hili limetokana na watanzania wenyewe kwa ajili ya kutatua chagamoto za watafiti hivyo hii ndio fursa ya watafiti kujiunga na ATARE,”amesema Profesa Nduguru.

Aliongeza kuwa “kupitia Chama hiki tutaweza kuibua fursa ikiwa ni pamoja kuishauri serikali,”aliongeza.

Rais wa ATARE Profesa Joseph Ndunguru ambaye pia ni mwazilishi wa Chama hicho akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utendaji wa Chama hicho