Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
WADAU Mkoani Tabora wamepongeza serikali ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha mpango maalumu wa kudhibiti maambukizi ya malaria nchini.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika semina ya siku moja ya kutambulisha mpango huo kwa wadau wa maendeleo Mkoani hapa, wamesema mkakati huo unaoenda sambamba na ugawaji vyandarua katika kaya utasaidia sana kupunguza vifo vitokanavyo na ugonjwa huo.
Chifu Msagata Fundikira (Chifu wa Wanyamwezi) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Machifu wote wa Mkoa wa Tabora amesema ugonjwa wa malaria bado ni tishio katika maeneo mengi ndani ya Mkoa huo.
Amebainisha kuwa wamepokea kwa mikono miwili mpango wa serikali wa kusajili kaya katika wilaya zote na kuzigawia vyandarua.
‘Chifu Mkuu Hangaya ambaye ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anajali sana afya za wananchi wake ndiyo maana ametenga fedha za kutosha ili kufanikisha mpango huu,’ ameongeza.
Chifu Fundikira ameasa jamii kutokwamisha mpango huo kwa kuingiza dhana mbaya na mila potofu juu ya matumizi ya vyandarua vyenye dawa watakavyogawiwa wananchi.
 Shekhe wa Mkoa wa Tabora, Shekhe Ibrahim Mavumbi ameeleza kuwa mpango huo utasaidia kuokoa watoto wenye umri wa kati ya miezi 6…59, wajawazito, wazee na makundi mengine ambayo yapo katika hatari kubwa ya kupoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.
Ameongeza kuwa ugonjwa huo ni hatarishi kwa nguvu kazi ya Taifa hivyo akaahidi kuwa wapo tayari kuunga mkono juhudi za serikali kwa kuelimisha waumini wao kwenye nyumba za ibada.
Akiongea kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo Mkuu wa Wilaya ya Tabora Luis Bura amesema katika kufanikisha mpango huo watagawa zaidi ya vyandarua mil 1.5 kwa kaya zaidi ya laki 4.
Pia watatoa Elimu ya afya na usafi wa mazingira ili kuondoa mazalia ya mbu, pia watatoa dawa za kinga na unyunyiziaji wa viuadudu ili kupunguza maambukizi ya ugonjwa huo hadi kufikia malengo ya Taifa ya chini ya asilimia 3.5 ifikapo 2025 na zero malaria ifikapo mwaka 2030.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa huo Dkt Honoratha Rutatinisibwa anafafanua kuwa Mkoa huo unaongoza kwa kuwa na kiwango kikubwa cha maambukizi ya ugonjwa wa malaria nchini kutokana na Utafiti wa mwaka 2022.
Ameeleza kuwa kiwango hicho kimepanda kutoka asilimia 11.7 mwaka 2017/2018 hadi kufikia asilimia 23.4 mwaka 2022 sawa na ongezeko la asilimia 50.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa