Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Wilbrod Mutafungwa amewaonya watu wanaofanya uhalifu ndani ya Ziwa Victoria ikiwemo uvuvi haramu huku akisisitiza kuwa jeshi hilo halita mvumilia mhalifu.
Kamanda Mutafungwa ametoa kauli hiyo leo Septemba 23, 2023 wakati akitoa elimu ya kuzuia uhalifu kwa wananchi wa Kata ya Bugogwa, Sangabuye, Shibula na Kayenze wilayani Ilemela mkoani hapa ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake yenye lengo la kutoa elimu ya kuzuia uhalifu kwa makundi mbalimbali ya wananchi.
Kupitia kikao hicho pia ametangaza wakati mgumu kwa wahalifu wanaopora vyavu za wenzao na mazao ya uvuvi huku akiahidi hatua kali za kisheria kuchukuliwa dhidi ya wahusika.
“Kuanzia leo msako mkali wa kuwasaka wahalifu katika maeneo yote unaendelea, watafute pa kwenda maana inakuja opereseheni kali ambayo itawapa wakati mgumu sana wahalifu,” amesema Mutafungwa
Huku akisisitiza ushirikiano kutoka kwa wananchi kwa maana mpaka sasa wana majina ya wahalifu hivyo watawafuata popote walipo iwe majini au nchi kavu.
Aidha ameomba ushiriki wa jamii kutokomeza vitendo hivyo kwani usalama wa nchi unalindwa na kila mwananchi ili kuwezesha shughuli za maendeleo kuendelea nchini.
“Wote kwa pomoja tunatakiwa kuwatambua watu wabaya na kuwatolea taarifa, ninyi ni watanzania lazima muwe wazalendo kwa nchi yenu,” amesisitiza Mutafungwa
Sanjari na hayo Kamanda huyo amekemea vitendo vya imani za kishirikina ikiwemo Kamchape na Lambalamba na kuwataka wanaoendesha shughuli hizo kujisalimisha wenyewe kwa jeshi hilo kabla hawajaanza kusakwa.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa